• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Wanafunzi wauawa Sudan wakilalamikia uhaba wa mikate

Wanafunzi wauawa Sudan wakilalamikia uhaba wa mikate

Na AFP na MARY WANGARI

WANAFUNZI wanne waliuawa kwa kupigwa risasi nchini Sudan mnamo Jumatatu katika maandamano ya kulalamikia dhidi ya uhaba wa mikate na mafuta huku uchumi wa taifa hiyo ukizidi kusambaratika.

Wanafunzi hao walikuwa miongoni mwa watu watano waliouawa katika eneo la Kaskazini la Kordofan mjini Al Obeid wakati wa maandamano kulalamikia upungufu mkubwa wa mikate na mafuta.

Waandalizi wa maandamano hayo wakiitisha mikutano kote nchini dhidi ya “mauaji hayo ya halaiki.”

“Shujaa watano walifariki kutokana na majeraha ya risasi wakati wa mkutano wa amani mjini Al-Obeid,” kamati ya madaktari inayohusishwa na kundi la waandamanaji ilisema kupitia taarifa.

“Waliofariki walijumuisha wanafunzi wanne wa shule za sekondari,” kiongozi maarufu wa maandamano hayo Babikir Faisal alisema.

Kufuatia kisa hicho, baraza la kijeshi linalotawala nchini humo limetangaza amri ya kutotoka nje usiku.

Mauaji haya yamejiri takriban miezi minane baada ya hali duni ya kiuchumi kuchochea maandamano ya raia wa Sudan yaliyosababisha kung’olewa mamlakani kwa kiongozi wa muda mrefu aliyekuwa rais Omar Al Bashir mnamo Aprili.

Baraza la jeshi ambalo limekuwa likitawala tangu Bw Al Bashir alipong’atuliwa kwenye urais pamoja na viongozi wa makundi ya waandamanaji walitarajiwa kukutana jana kwenye awamu mpya ya mazungumzo kuhusu mustakabali wa serikali ya nchi hiyo.

Mkataba

Mapema Julai, baraza la kijeshi pamoja na waandamanaji waliingia kwenye mkataba wa kugawana mamlaka na kuunda utawala wa pamoja kwa lengo la kuongoza taifa katika utawala wa raia siku zijazo japo kuna masuala tele ambayo bado hayajasuluhishwa.

Licha ya mazungumzo hayo, bado kumekuwa na hali ya taharuki kati ya vikosi vya kijeshi na waandamanaji kufuatia msako wa Rapid Support Forces, ambalo ni kundi la wapiganaji linaloungwa mkono na serikali, katika kambi ya waandamanaji mnamo Juni 3, 2019, uliosababisha vifo vya watu 127.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na waendeshaji mashtaka pamoja na baraza la kijeshi ulisema kwamba ni watu 17 pekee waliouawa mnamo Juni 3 huku 87 wakiuawa kati ya tarehe hiyo na Juni 10.

Ripoti hiyo iliwatambulisha maafisa 8 waliohusika katika msako huo wa kikatili katika kambi ya waandamanaji, wakiwemo maafisa watatu kutoka kundi la Rapid Support Forces, lakini baraza la kijeshi lilisisitiza halikutuma kundi hilo la wapiganaji kutawanya kikao hicho.

Waandamanaji, hata hivyo, wamekataa matokeo hayo na kuitisha uchunguzi usioegemea upande wowote.

Mjumbe wa Marekani nchini humo Bw Donald Booth amelionya baraza la kijeshi kwamba haijalishi uchunguzi wao utakuwa makini kiasi gani, kwa sababu bado watakabiliwa na maswali kuhusu ukweli wa matokeo yake ikizingatiwa uwezakano wa mchango wao katika uvamizi huo.

You can share this post!

Masoud Juma asajiliwa sasa nchini Algeria

Idadi ya waliouawa kwenye shambulizi la Boko Haram...

adminleo