• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Wanajeshi wa zamani waunga maandamano kupinga serikali

Wanajeshi wa zamani waunga maandamano kupinga serikali

Na AFP

BEIRUT, LEBANON

MAELFU ya raia wa Lebanon wakiongozwa na wanajeshi wa zamani, wikendi walivamia afisi ya Wizara ya Masuala ya Kigeni na kuigeuza makao makuu ya uanaharakati kutokana na kukasirishwa na kile walikiita ni utepetevu wa serikali kufuatia mlipuko mkubwa uliotokea Beirut wiki jana.

Waandamanaji hao pia walivamia afisi kadhaa za serikali zikiwemo zile za Chama cha benki nchini humo na kuzikiteketeza kabisa. Afisi za wizara za Uchumi na Mazingira pia zilivamiwa na raia ambao wanapigania uongozi wa Waziri Mkuu Hassan Diab ung’olewe mamlakani.

Mlipuko jijini Beirut ulitokea siku sita zilizopita na kusababisha uharibifu mkubwa wa majengo pamoja na vifo vya zaidi ya watu 160.

Saa chache baada ya maandamano hayo kuanza jijini Beirut, Diab aliahidi kuandaa uchaguzi mapema huku wito ukitolewa wa kumtaka ajiuzulu pamoja na maafisa wanaohudumu katika serikali yake.

Waziri huyo mkuu naye aliahidi kubuni sheria zitakazowezesha taifa hilo kuandaa uchaguzi wake mapema na akaahidi kusalia uongozini kwa miaka miwili pekee hadi vyama vyote viafikiane kuhusu tarehe ya kura hiyo.

Kwenye maandamano ya wikendi, polisi walilazimika kutumia vitoa machozi na kufyatua risasi hewani kuwatawanya raia waliokuwa wakiteketeza afisi za serikali.

Cha kushangaza ni kwamba, hawakuteketeza afisi za masuala ya kigeni ila wakaigeuza makao makuu ya mchakato wa mageuzi waliouanzisha.

Wingu la moshi lilitanda kotekote huku maelfu ya waandamanaji wakitawanyika hadi viungani mwa mji wakikwepa polisi na pia kuwashambulia.

Maandamano hayo yametajwa kuwa hatari zaidi baada ya yale ya kitaifa ya Oktoba mwaka uliopita ambapo raia walipigania kuondolewa kwa serikali mamlakani kutokana na uongozi mbaya.

Jumapili, ubalozi wa Amerika uliwaunga mkono raia wa Lebanon katika vita kati yao na serikali.

“Raia wa Lebanon wameteseka sana na ni vyema iwapo viongozi wao watawasikiza. Serikali inafaa kuendesha shughuli zake kwa uwazi na kuitikia wito wa raia kuwe na mabadiliko. Tunawaunga mkono wakiandamana ila tunawaomba wajiepushe na ghasia,” ikasema taarifa kutoka ubalozi huo.

Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu nchini humo, mwanajeshi mmoja alifariki huku wengine 200 wakijeruhiwa wakiwemo 63 waliohamishwa kupokea matibabu hospitalini.

  • Tags

You can share this post!

Sonko, Badi wazidi kuvutania ukusanyaji kodi

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kiswahili kama fumbato la...

adminleo