Kimataifa

Wanaoshiriki ngono na wageni walaumiwa kueneza Covid-19 Australia

July 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MARY WANGARI

MAAFISA nchini Australia wameanzisha uchunguzi huku kukiwa na madai kuwa mkurupuko mpya wa virusi vya corona eneo la Victoria ulisababishwa na baadhi ya wafanyakazi wanaokaidi kanuni.

Imedaiwa kwamba baadhi ya wanakandarasi hawafuati masharti katika hoteli moja inayotumiwa kama karantini kwa wageni wa kimataifa, ikiwemo kushiriki ngono na watu waliotengwa.

Vyombo vya habari nchini humo zimetangaza kuwa serikali nchini humo itatoa Sh319.5 milioni kufadhili uchunguzi huo

Awali iliripotiwa kuwa visa kadhaa mwishoni mwa Mei na mapema Juni huenda vikahusishwa na “kukaidi kanuni za kudhibiti maambukizi katika mpango wa karantini hotelini humo.”

Mamlaka imechukua usukani wa hoteli kadhaa kote nchini humo kama sehemu ya mikakati yake kabambe ya kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.

Yeyote anayewasili Australia ni sharti akae karantini kwa muda wa siku 14 katika vituo hivyo vinavyosimamiwa na serikali.

Ni raia wa Australia pekee na wakazi wa kudumu wanaoruhusiwa kuingia nchini humo na wengine wachache.

Ripoti nchini humo ziliashiria kuwa visa 31 zimehusishwa na hoteli ya Melbourne’s Stamford Plaza, huku vingine vikihusishwa na hoteli ya Rydges on Swanston ambayo pia iko katika jiji kuu nchini humo.

“Ni bayana kabisa kwamba kile kimetokea hapa si sawa kamwe na tunahitaji kujua ni nini hasa kimetendeka,” ilisema taarifa.