Wanasayansi sasa wadai bangi inaongeza nguvu za kiume
MASHIRIKA Na PETER MBURU
HISTORIA ya kuvuta bangi, hata ikiwa mtu aliitumia mara moja, imebainika kuongeza nguvu za uzazi kwa kiwango kikubwa miongoni mwa wanaume, hata ikiwa mtu aliwacha kuitumia.
Hii ni kulingana na utafiti uliofanywa na wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Hrvard, walipokuwa wakipima idadi ya manii miongoni mwa zaidi ya wanaume 600, kati ya wanandoa waliohudhuria kliniki ya uzazi.
Japo wanasayansi walitarajia utumiaji wa bangi uwe unaathiri ubora wa uzalishaji kwa kupunguza idadi ya manii miongoni mwa wanaume wanaotumia, walishangaa walipobaini kuwa kinyume na matarajio yao, bangi inaboresha hali. Walibaini kuwa wanaume wanaotumia bangi walikuwa na kiwango cha juu cha uzazi, ikilinganishwa na wasiotumia.
Wanasayansi sasa wanasema kuwa utumiaji wa dawa hiyo ya kulevya unaongeza homoni za kiume ziitwazo Testosterone na pia kumfanya mtumiaji kuwa tayari zaidi kufanya kitu cha kuhatarisha maisha.
Mtafiti mkuu Dkt Jorge Chavarro alisema kuwa “Matokeo haya ambayo hatukutarajia yanadokeza kuhusu mambo ambayo hatukufahamu kuhusu umuhimu wa bangi katika suala la uzazi, ama faida zoke kwa jumla.”
Hata hivyo, wanasayansi hao walisema kuwa utafiti zaidi unahitajika, ili kubaini faida zingine za bangi kwenye afya ya binadamu.
Tafiti za mbeleni ambazo zilihusisha wanyama kama sampuli zilisema kuwa matumizi ya bangi yanaathiri afya ya uzazi ya wanaume.
Katika utafiti huu, wanasayansi walikusanya sampuli 1, 143 za manii kutoka kwa wanaume 662 katika kipindi cha 2000 na 2017.
Kwa kadri, wanaume walikuwa wa miaka 36, wengi wakiwa wazungu na watu waliosoma. Wote walihusisha wanandoa waliokuwa wakitafuta usaidizi katika kliniki ya uzazi ama nguvu za uzazi. Watu hao walihitajika kujaza fomu ambapo walieleza kuhusu historia yao ya matumizi ya bangi.
Zaidi ya nusu kati yao waliripoti kuwahi kutumia bangi wakati fulani maishani. Asilimia 44 kati yao walisema kuwa waliwahi kutumia dawa hiyo mbeleni, nao asilimia 11 wakajitaja kuwa watumizi hadi wakati huo wa utafiti.
Uchunguzi wa sampuli za manii ulionyesha kuwa wanaume waliokuwa wamevuta bangi walikuwa na kiwango cha manii cha milioni 62.7 kwa kadri kwa kila milimita, ilhali wale ambao hawajawahi kuvuta walikuwa na milioni 45.4.
Ni asilimia 5 tu ya watumiaji wa bangi ambao kiwango chao cha manii kilikuwa chini ya milioni 15, ambacho ndicho kiwango cha kawaida kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), ikilinganishwa na asilimia 12 ya wanaume ambao hawakuwa wamewahi kutumia dawa hiyo.
Wanasayansi hao aidha walibaini kuwa matumizi ya bangi yanaongeza kiwango cha homoni ya Testosterone ambayo hupatikana ndani ya wanaume.
Wanasayansi walisema kuwa kemikali inayopatikana akilini inayoitwa endocannabinoid na ambayo hulengwa na bangi mtu anapoivuta inajulikana kupima ubora wa uzalishaji ndani ya mwanamume.
Wanasayansi, hata hivyo, walisema kuwa si lazima utumiaji wa bangi uwe ndio unachangia wanaume kuwa na kiwango kikubwa cha homoni Testosterone na kufanya mambo ya kuhatarisha, ila kinyume chake, wingi wa homoni hizo unaweza kumfanya mtu aidha kufanya tabia za kuhatarisha kama kuvuta bangi.
Matokeo hayo yaliungwa mkono na mtaalam kutoka Uingereza, Profesa Allan Pacey, ambaye alisema “wanaume walio na idadi kubwa ya manii wanaweza kuwa na kiwango kikubwa cha Testosterone na pia kufanya mambo ya kuhatarisha kama kuvuta bangi.”