Wanasayansi wavumbua dawa ya kuondoa usahaulifu
MASHIRIKA Na PETER MBURU
WANASAYANSI wametengeneza dawa ambayo inalenga kuondoa usahaulifu kwenye akili, hali inayokumba watu wanapofika umri wa makamo na kuendelea, ambayo itaanza kufanyiwa majaribio kwa binadamu hivi karibuni.
Ikifanikiwa, ikiwa huwa unasahau mambo madogomadogo kama ulipoweka funguo, kuwasahau watu ama mahali ni mambo ambayo utayazika kwenye kaburi la sahau.
Utafiti umeonyesha kuwa hali ya usahaulifu ambayo imekuwa ikihusishwa na uzee kuja inaweza kuondolewa kwa matumizi ya dawa hiyo ambayo inarejesha seli za akili katika hali yake ya siku za ujana.
Inatarajiwa kuwa utafiti huo utatoa dawa za kila siku ambazo zitawafaa wazee kulainisha akili zao na kutibiwa kutokana na hali ya usahaulifu.
Majaribio ya dawa hiyo kwa binadamu yanatarajiwa kufanywa ndani ya miaka miwili.
Tayari dawa yenyewe imefanyiwa majaribio dhidi ya panya, ambao miili yao inawiana na ya binadamu kabisa, na ikafanya kazi vyema. Walipopewa, panya wazee waliimarika kiakili na kuonekana kama wenzao wadogo.
Mtafiti Mkuu Dkt Etienne Sibille alisema “kwa sasa hakuna dawa za kutibu ishara za usahaulifu wa akili ambazo hutokea wakati mtu akiwa na mawazo mengi, uzeeni ama magonjwa mengine ya akili.”
“Utafiti wetu unahusiana na hali ya watu kusahau katika uzee wa kawaida moja kwa moja. Hii inaweza kuhusiana na masomo na akili, ufafanyaji wa maamuzi na kupanga mambo,” akasema Dkt Sibille.
Dawa hiyo itajaribiwa kwa watu wazima wenye mawazo na usumbufu wa kiakili, kisha wazee wanaokumbwa na shida ya kusahau.
“Itakuwa ikitumiwa dawa moja kwa siku,” akasema.
Ilipofanyiwa majaribio dhidi ya panya, dawa hiyo ilifanya kazi ndani ya dakika 30 na kuonyesha kazi nzuri kwa asilimia 80.
Baada ya kupewa dawa hiyo kila siku kwa miezi miwili, akili za panya hao ambao walikuwa na mawazo mengi ya uzeeni zilirejea katika hali ya ujana na panya wakachangamka.