Kimataifa

‘Wantam’ au ‘Tutam’? Rais Chakwera wa Malawi kujua mbivu na mbichi kura zikihesabiwa

September 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BLANTYRE, MALAWI

RAIA wa Malawi sasa wanasuburi kujua kiongozi wao baada ya kupiga kura kwenye uchaguzi ambao uliandaliwa Jumanne.

Wapigakura Malawi walielekea debeni kwenye uchaguzi ambao ushindani mkali unatarajiwa kati ya Rais Lazarus Chakwera,70 na mtangulizi wake Peter Mutharika, 85.

Kiongozi mpya anatarajiwa kupambana na mfumko wa uchumi na kuongezeka kwa bei ya chakula, hali ambayo imefanya maisha kuwa magumu.

Mbali na wawili hao, uchaguzi huo uliwashirikisha wawaniaji wengine 15 akiwemo Rais wa zamani Joyce Banda.

Katiba ya Malawi inasema kuwa mshindi anastahili kutangazwa katika muda wa wiki moja kwa hivyo matokeo huenda yakatangazwa wiki hii.

Iwapo hakutakuwa na mshindi ambaye atapata asilimia 50 za kura, basi kutakuwa na duru ya pili ambapo mshindi na atakayeibuka wa pili watachuana tena.

Baadhi ya wapigakura walieleza imani kuwa wamempigia kura mwaniaji ambaye atawasaidia kusuluhisha changamoto tele zinazozonga nchi hiyo.

“Nimempigia mwaniaji ambaye nina matumaini atasaidia kusuluhisha tatizo la njaa. Kwa sasa napambana kuwakimu watoto wangu,” akasema Alindiine Bellison Kazembe, 32 ambaye ni mama wa watoto wanne na ni mjakazi jijini Blantyre.

Malawi imekumbwa changamoto tele za kiuchumi tangu Chakwera ambaye alikuwa mhubiri, achaguliwe mnamo 2022.

Kimbunga cha mara kwa mara na ukame umechangia mimea kutofanya vizuri nao mfumko wa uchumi umekwepo kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

“Nimepiga kura nikiwa na matumaini kuwa rais anayekuja atatusaidia kuboresha uchumi wetu,” akasema Mazaza Masika, 50.

Masika alisema alipoteza kazi yake wakati wa janga la corona na bado hajapata ajira tangu wakati huo.

Jumanne vituo vya upigaji kura vilifunguliwa saa 12 asubuhi japo watu walichelewa kupiga kura katika baadhi ya vituo kutokana na teknolojia ya kutambua vidole vyao kukosa kufanya kazi.

Ilibidi raia wapige kura kwa njia ya kawaida kwenye baadhi ya vituo baada ya mitambo hiyo ya kielektroniki kufeli.