Kimataifa

Wanyoa nywele kupinga kuteuliwa kwa Cho Kuk kuwa waziri

September 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

SEOL, Korea Kusini

KIONGOZI wa upinzani Korea Kusini ndiye mbunge wa hivi majuzi kunyoa nywele yake hadharani akilalamikia serikali.

Hwang Kyo-ahn, alinyoa nywele zake zote kichwani mbele ya wafuasi wake na vyombo vya habari nje ya Ikulu ya rais mnamo Jumatatu jioni.

Malalamishi hayo ni kuhusu waziri mpya wa haki, Cho Kuk, ambaye familia yake imeandamwa na madai ya ufisadi.

Juma lililopita, wabunge wawili wa kike walinyoa nywele kwenye vichwa vyao kuhusu suala hilo lenye utata.

Wabunge hao watatu wote ni wa mrengo wa kisiasa unaopinga serikali iliyopo inayoongozwa na Rais Moon Jae-in, wanaolalamika wakitaka Cho ama ajiuzulu au apigwe kalamu.

Cho Kuk aliyekuwa profesa wa sheria na msaidizi wa Rais Moon, alichukua usukani wiki iliyopita kama waziri wa haki.

Lakini wakosoaji wake wameghadhabishwa na kwamba aliteuliwa katika wadhifa huo na Bw Moon licha ya shutuma zinazoendelea kuhusu udanganyifu wa elimu na hatia za kifedha dhidi ya familia yake.

Mkewe, ambaye pia ni profesa wa sheria, ameshtakiwa kwa madai ya kughushi stakabadhi iliyomwezesha bintiye kujiunga na chuo kikuu na kupata udhamini wa elimu, jambo ambalo limewahamakisha wanafunzi wengine wa chuo kikuu.

Korea Kusini ina utamaduni wa jadi wa kunyoa nywele kama mbinu ya kulalamika.

Kitendo hicho kimejikita katika mafunzo ya kitamaduni na kihistoria kimeonekana kama njia ya kuashiria kuhusu msimamo fulani.

Uasi

Miaka ya sitini na sabini, Korea Kusini ilipokuwa katika utawala wa kiimla, waasi walinyoa nywele kwenye vichwa vyao kama ishara ya uasi.

Katika miongo iliyopita, wanaharakati na wanasiasa wametumia kitendo hicho kama njia ya kuashiria malalamishi yao.

Mnamo 2018, wanawake walinyoa vichwa vyao dhidi ya kuongezeka kwa kamera za ujasusi zilizokuwa zikiwekwa vyooni na vyumba vya kubadilishia nguo ili kuwarekodi kisiri wanawake.

Miaka miwili iliyotangulia, raia zaidi ya 900 wa Korea walinyoa vichwa vyao katika ishara ya kulalamikia dhidi ya mfumo wa Amerika wa kupinga roketi za kivita.

Mnamo 2007, mamia ya wakazi wa Jiji la Icheon walinyoa vichwa vyao kuhusiana na utata wa eneo la kujengewa kiwanda.