Wapalestina waomboleza ulimwengu ukisherehekea Sikukuu ya Eid-al-Adha
NA MASHIRIKA
GAZA, UPALESTINA
RAIA wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na eneo lililotekwa la West Bank wanaadhimisha Sikukuu ya Eid al Adha iliyojawa na huzuni huku jeshi la Israeli likiendeleza mashambulizi yake hatari zaidi ya miezi minane tangu vita hivyo vilipoanza.
Jana watu walikusanyika ili kusali kwenye vifusi karibu na maeneo yao katika sehemu iliyozingirwa ambapo Wapalestina zaidi ya 37,000 wameuawa.
Haya yanajiri huku jeshi la Israeli likizidisha mashambulizi katika maeneo ya Magharibi mwa Rafah huku likiendeleza uvamizi wake ardhini mwa mji wa kusini na kushambulia maeneo katikati mwa Gaza.
Kituo cha habari cha serikali Gaza kilisema kupitia taarifa Jumamosi kuwa Israeli inazuia kuingizwa kwa wanyama wa kutolewa kafara katika eneo lililotekwa kutoka vivuko vyote hivyo kuzuia Wapalestina kufanya matambiko ambayo ni sehemu ya Eid al-Adha.
Jeshi la Israeli jana lilitangaza ‘mikakati ya kusitisha’ shughuli za kijeshi katika mkondo mojawapo kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa moja usiku kila siku hadi notisi nyingine itakapotolewa ili kuruhusu msaada zaidi kuingia Gaza kutoka kwenye kivuko cha Karem Abu Salem (Kerem Shalom).
Hata hivyo, ilisisitiza kuwa wanajeshi wake wataendelea na mapigano katika sehemu ya kusini mwa Gaza na kwamba ‘vita havitasitishwa’.
Waziri wa Usalama Israeli anayeegemea mrengo wa kulia, Itamar Ben-Gvir, alipuuzilia mbali hatua hiyo ya kusitisha mapigano kama ya ‘isiyo na urazini’ hasa baada ya wanajeshi 10 wa Israeli kuuawa Jumamosi, siku iliyoandikisha idadi kubwa zaidi ya vifo vya wanajeshi wa Israeli tangu Januari.
Jijini Jerusalem, vikosi vya Israeli kwa mara nyingine vilivamia Wapalestina waliokuwa wanajaribu kuadhimisha sherehe za Eid al-Adha katika Msikiti wa Al-Aqsa Mosque, huku jeshi likiweka masharti makali kuhusu kuingia na kuwashambulia waumini.
Ripoti ziliashiria kuwa watu 40,000 waliweza kuhudhuria maombi ndani ya msikiti huo lakini wengi walilazimika kusali nje ya malango ya misikiti baada ya kuzuiwa kuingia.
Iliripotiwa vilevile kuwa vikosi vya Israeli vilikatiza safari za Wapalestina katika maeneo kadhaa kote Ramallah katika jiji lililotekwa la West Bank, huku vikiweka vituo vya ukaguzi na kushurutisha magari kusimama.
Maafisa wawili wakuu wa Umoja wa Mataifa wenye makao yao nchini Lebanon wameonya kuhusu tishio ‘halisi’ la hitilafu ambayo huenda ikasababisha vita vikubwa kwa sababu majeshi ya Israeli na Hezbollah yamezidisha makali ya mashambulizi yake katika mapigano mpakani yaliyozuka baada ya michafuko kuzuka Gaza.
“Huku jamii nchini Lebanon na kote duniani zinaposherehekea Eid al-Adha, familia ya UN inasisitiza wito wake kwa wahusika wote kwenye Mpaka wa Blue Line, kuweka chini silaha zao na kujitolea kufuata mkondo wa amani,” walisema maafisa hao katika taarifa ya pamoja.