Washirika zaidi wa Trump waambukizwa Covid-19
Na MASHIRIKA
WASHINGTON DC, Amerika
MAAMBUKIZI ya corona yanaendelea kuitikisa serikali ya Rais Donald Trump wa Amerika, baada ya washirika wake wa karibu pia kubainika wameambukizwa hapo jana Jumatano.
Miongoni mwa wale waliobainika kuambukizwa ni Mshauri Mkuu wa Ikulu ya White House, Stephen Miller na afisa mmoja wa kijeshi wa ngazi za juu.
Viongozi kadhaa wa kijeshi pia wamewekwa kwenye karantini, baada ya Naibu Kamanda katika Jeshi la Maji, Charles Ray, kuthibitishwa kuwa na virusi hivyo.
Washirika wengine wa karibu wa Trump waliothibitishwa kuambukizwa virusi hivyo ni msaidizi wake, Hope Hicks, Seneta Mike Lee (wa chama cha Republican), msaidizi wake wa kibinafsi Nicholas Luna kati ya wengine.
Licha ya Rais Trump kutangaza kuwa amepona siku chache baada ya kuthibitishwa kuambukizwa, mwaniaji urais wa chama cha Democratic, Joe Biden, amesema kuwa kiongozi huyo hapaswi kushiriki kwenye mjadala wa urais ikiwa bado ana virusi.
Akizungumza kuhusu duru ya pili ya mdahalo huo unaotarajiwa kufanyika Alhamisi ijayo mjini Miami, Florida, Biden alisema atazingatia ushauri atakaopewa na madaktari.
“Nadhani bado ana virusi vya corona. Hatupaswi kushiriki kwenye mdahalo huo,” akasema.
Trump alirejea katika Ikulu kutoka hospitalini Jumatatu baada ya kuthibitishwa kuambukizwa covid-19 wiki iliyopita.
Alilazwa katika hospitali ya Walter Reed Medical Centre, aliyoisifu kwa “kumpa matibabu mazuri.”
Miller alisema kuwa yuko kwenye karantini “baada ya kutobainika kuwa na virusi licha ya kupimwa mara kadhaa.” Alisema atakuwa kwenye karantini hadi Jumanne ijayo.
Alikuwa ameshiriki hafla pamoja na Rais Trump siku moja baada yake kuthibitishwa kuambukizwa.
Wawili hao pia walisafiri pamoja kwenye Ndege ya Airforce One mnamo Septemba 27, kwa mujibu wa ripoti za gazeti la ‘New York Times.’
Mkewe Miller, Katie Miller, alithibitishwa kuambukizwa virusi mnamo Mei, lakini akapona baadaye.
Katie ndiye msemaji rasmi wa makamu wa rais wa Trump, Mike Pence.
Mwezi Julai, nyanyake Miller, Ruth Glossler, 97, alifariki kutokana na kile kilichotajwa kuwa “athari za virusi vya corona.”
Hata hivyo, Ikulu ilikanusha madai hayo, badala yake ikisema “alifariki kutokana na matatizo ya uzee akiwa usingizini nyumbani kwake.”
Licha ya hayo, mjombake Miller alitoa cheti kilichoonyesha marehemu alifariki kutokana na “matatizo ya kupumua.”