Kimataifa

Watafiti wadai corona yaweza kusambazwa kupitia kupumua

April 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

VIRUSI vya corona vinaweza kusambaa hewani mwathiriwa anapopumua au kuongea kama kawaida, mwanasayansi mmoja wa Amerika amesema. Na saa chache baada ya Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Kuambukiza katika Taasisi ya Kitaifa kuhusu Afya (NIH) Anthony Fauci kutoa kauli hiyo, Rais Donald Trump aliwashauri wananchi wote kuvalia barokoa nyakati zote.

Hii ni baada ya Amerika kuvunja rekodi ya dunia kwa kuthibitisha vifo vya wagonjwa 1,480 kutokana na Covid-19 ndani ya saa 24. Profesa Fauci alisema utafiti umebaini kuwa virusi hivyo vinaweza kusambaa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia mazungumzo ya kawaida kando na kukohoa au kupiga chafya.

Kabla ya mtaalamu huyo kutoa ufichuzi huo, mwongozo rasmi ulisema kuwa ni wagonjwa pekee wanapaswa kufunika mapua na midomo yao pamoja na wale wanaowatunza nyumbani au hospitalini.

Kauli ya Fauci imejiri baada ya Shirika la Kitaifa la Sayansi (NAS) kutuma barua katika Ikulu ya White House mnamo Aprili 1 likitoa maelezo kuhusu utafiti mpya kuhusu suala hilo. Lilisema japo utafiti haujakamilishwa, “matokeo yaliyoko yanaonyesha kuwa virusi vya corona vyaweza kusambazwa kwa kupumua kawaida.”

Hadi kufikia Ijumaa, taasisi za kiafya nchini Amerika zilishikilia kuwa virusi hivyo hupitishwa kwenye matone madogo madogo ambayo hutoa mgonjwa anapopiga chafya au kukohoa

Matone hayo yanaweza kuanguka haraka umbali wa mita moja kutokana mahala alipo mwathiriwa huyo.

Lakini ikiwa virusi hivyo vinaweza kutolewa pale mgonjwa anapopumua kwa njia ya kawaida, itakuwa vigumu kuvidhibiti kusambaa kwavyo.

“Hii ndio maana ni muhimu kwa kila mtu kufunika midomo na mapua yao kwa kutumia barokoa,” akaeleza Profesa Fauci. Kauli hii inalandana na ushauri uliotolewa na Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe kwamba, wahudumu wa magari ya uchukuzi, bodaboda na tuk tuk wanahakikishe kuwa wao na abiria wao wamevalia vifaa hivyo nyakati zote.

Matokeo ya utafiti yaliyochapishwa juzi katika Jarida la kimatibatu la “New England Journal of Medicine” ilifichua kuwa virusi vya corona vinaweza kusalia hewani kwa hadi saa tatu.

Hata hivyo, kufikia sasa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) halijakubaliana kamili na kauli za wanasayansi kwamba virusi hivyo vinaweza kusambaa hewani mgonjwa anapopumua au kuongea.

Katika uchanganuzi wake uliochapishwa mnamo Machi 29, shirika hili lilisema kuwa, kusambaa kwa virusi vya corona kwa njia hiyo kunaweza kutokea tu wakati mgonjwa anatibiwa, ambapo husaidiwa kupumua.