Watawa wakiri kuiba mamilioni na kuyatumia kucheza kamari
NA MASHIRIKA
WATAWA wawili wa Kanisa Katoliki wamekiri kuiba Sh50 milioni kutoka katika shule inayomilikiwa na kanisa hilo jimboni California na kwenda kuzitumia kucheza kamari mjini Las Vegas, Amerika.
Watawa hao Mary Kreuper na Lana Chang waliiba fedha hizo kutoka shule ya St James Catholic ambapo walikuwa wakifanya kazi mjini Torrance na kuzitumia katika kamari.
Wawili hao ambao walistaafu hivi karibuni, wakidaiwa kuwa marafiki wa karibu walichukua fedha ambazo zilikuwa ada ya wanafunzi.
Mary Kreuper alikuwa mkuu wa shule hiyo kwa miaka 29 na Lana Chang alifundisha shuleni humo kwa karibu miaka 20.
Walimu hao walikiri kuiba fedha za shule kwa kipindi cha miaka 10 waliyokuwa shuleni hapo.
Jumatatu, shule ya St James Catholic ilisema kuwa watawa hao wamejutia wizi huo na hawatafikishwa mahakamani.
“Watawa hao wamekiri kufuja fedha za shule na wameshirikiana vyema na maafisa wa uchunguzi,” ikasema taarifa ya shule hiyo. Watawa hao pia wameandikia shule hiyo barua wakiomba radhi kwa kufuja fedha.
Msimamizi wa Parokia Michael Meyers aliandikia barua shule hiyo akisema: “Mary Margaret na Sister Lana wamejutia uoavu waliotekeleza na ninaomba muwasamehe”.
Parokia Kuu ya Los Angeles ilisema kuwa ilibaini kwamba fedha hizo zilipotea wakati wa kufanya ukaguzi wa hesabu.