Kimataifa

Watoto wa Mr Ibu waiba Sh9.9m za kugharimia matibabu yake

January 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

LAGOS, NIGERIA

WANA wawili wa mwigizaji staa wa Nigeria, John Okafor almaarufu Mr Ibu, walikamatwa kwa madai ya kuiba pesa zilizochangishwa kwa bili ya hospitali ya baba yao mwaka 2023.

Mr Ibu,62, alikatwa mguu Novemba 2023 baada ya mashabiki kuchanga pesa za kufadhili upasuaji huo.

Mwanawe wa kiume Daniel Okafor na bintiye wa kulea Jasmine Chioma wametuhumiwa kwa kudukua simu ya baba yao na kutwaa Sh9.9 milioni.

Kufikia sasa wawili hao hawajazungumza lolote tangu kukamatwa kwao katika mji wa Lagos.

Polisi walitoa taarifa kuhusu kukamatwa kwao na uchunguzi kuanzishwa kuhusu madai hayo ya ulaghai, baada ya wawili hao kuhudhuria kikao cha dhamana kortini Alhamisi.

Korti iliruhusu waachiliwe huru kwa bondi ya Sh2.7 milioni au wasalie kizuizini wakishindwa kulipa.

Kitengo cha upelelezi wa jinai kilieleza kuwa washukiwa waliweka programu kwenye simu ya baba yao baada ya kuanzisha mchango wa pesa za kulipia bili ya hospitali ya Mr Ibu.

Programu iliwawezesha kuhamisha pesa kutoka akaunti ya baba yao.

Wawili hao watarejea kortini Machi 11, 2024, kusikilizwa tena kwa kesi.

Matatizo ya kiafya ya Mr Ibu yalijulikana kwa umma Oktoba 2023 baada ya familia kuchapika video katika mitandao ya kijamii ya nyota huyo wa Nollywood akiwa hospitalini.

Aliomba mashabiki msaada wa bili ya matibabu na mwezi Novemba alifanyiwa upasuaji. “Baba amefanyiwa upasuaji na umefaulu.

Kuzidisha uwezekano wa kupona ilibidi mguu mmoja ukatwe,” lilisema chapisho kwenye Instagram.

Mr Ibu anafahamika kwa filamu za vichekesho na amedumu katika uigizaji kwa zaidi ya miongo miwili.

Mwigizaji huyo alipata umaarufu miaka 20 iliyopita katika filamu ya vichekesho ya Nigeria, na alijulikana na jina lake la utani la Mr Ibu.

Kufikia sasa filamu hiyo bado inachukuliwa kuwa mojawapo ya maonyesho bora zaidi ya Nigeria.

Mr Ibu aliendelea kuigiza katika sinema nyingine kadhaa maarufu za Nollywood, katika tasnia ya filamu ya mabilioni ya dola ya Nigeria inavyojulikana, katika kazi ambayo imechukua zaidi ya miongo miwili.

Nyota huyo aliliambia gazeti la hapa nchini miaka michache iliyopita kuwa alikuwa na jumla ya watoto 13 ambao baadhi yao waliasiliwa.