Watu 100 watuma maombi ya kazi ya kuua wahalifu
MASHIRIKA Na PETER MBURU
ZAIDI ya watu 100, wakiwemo wanawake wawili walituma maombi ya kazi ya kuua wahalifu nchini Sri Lanka, wakati serikali ya taifa hilo ilichapisha kuwa inawatafuta wafanyakazi wawili wa kazi hiyo.
Serikali ilitoa tangazo hilo, kutokana na makosa ya hukumu ya kifo, ambapo hakujakuwa na wafanyakazi wa kuua wahalifu korti zinapohukumu watu.
Rais Maithripala Sirisema alitangaza kuwa watu wanne ambao walihukumiwa kwa makosa yanayohusiana na mihadarati watakumbana na hukumu ya kifo, ndipo serikali ikaamua kuajiri watu wa kazi hiyo.
Hii ni baada ya miaka 43 bila ya yeyote anayehukumiwa kifo kuuawa nchini humo.
Kunyongwa kwa wanne hao kutakamilisha marufuku ya hukumu hiyo, ambayo imekuwepo tangu 1976.
Zaidi ya watu 100 walituma maombi baada ya serikali kuchapisha katika gazeti Februari. Wanaowasilisha maombi walihitajika kuwa raia wa nchi hiyo, wa kiume, wa kati ya miaka 18 hadi 45, na thabiti kimawazo.
Hata hivyo, wanawake wawili pia walituma maombi, japo hawakufanikiwa. Shirika la habari la Daily News ndilo liliripoti kuwa watu wawili raia wa Amerika na wanawake wawili walituma maombi.
Msemaji wa magereza alisema wawili waliofuzu watapata mafunzo ya wiki mbili kabla ya kuanza kazi.