Watu 22 wafariki huku zaidi ya 1,015 wakijeruhiwa baada ya tetemeko la ardhi Uturuki
Na MASHIRIKA
WATU 22 wamefariki huku zaidi ya 1,015 wakijeruhiwa baada ya tetemeko la ardhi la kipimo cha 6.8 kukumba maeneo ya Mashariki nchini Uturuki kando na kuporomosha majengo kadhaa karibu na eneo la mkasa, imethibitisha Wizara ya Masuala ya Ndani.
“Watu wanne wamefariki mjini Doganyol, Malatya na 18 wa kutoka Elazig nao wakiangamia,” amesema waziri Suleyman Soylu akihutubia wanahabari ambapo alikuwa pamoja na Waziri wa Afya na Mazingira na Ustawishaji Miji mkoani Elazig.
Angalau watu 39 wameokolewa kutoka kwa vifusi vya majengo eneo la mkasa.
Tetemeko hilo lenye nguvu lilisikika pia katika mataifa jirani yakiwemo Syria na Georgia.
Wahanga wengi ni wa kutoka katika mji wa Elazig. Vilevile wengine ni wa kutoka Malatya, kwa mujibu wa waziri wa afya wa Uturuki Fahrettin Koc.
Waziri wa mashauri ya ndani wa taifa hilo Suleyman Soylu amesema waokoaji wanawasaka manusura kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka.
Mamlaka ya kukabiliana na mikasa na hali za dharura ya taifa hilo imesema kuna uwezekano wa kutokea matetemeko mengine madogo baadaye katika eneo la mkasa.