Kimataifa

Watu 41 wafa katika ndege ya Urusi, 37 wakwepa kifo

May 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

WATU 41 waliaga dunia ndege ilipoteketea ilipokuwa ikitua kwa dharura katika uwanja wa ndege wa Sheremetyevo jijini Moscow baada ya kukumbwa na hitilafu.

Kanda za video zilizotumwa katika mitandao ya kijamii ziliwaonyesha wasafiri wakitumia milango ya kujiokoa kutokana na dharura kutoroka mauti kutokana na moto uliokuwa ukichoma ndege hiyo.

Kulingana na mashirika ya habari nchini Urusi, kati ya waliofariki ni watoto wawili na mhudumu wa ndege.

Ndege hiyo ilikuwa imebeba wasafiri 73 na wahudumu watano ilipopata ajali.

“Watu 37 waliepuka kifo; wakiwa wasafiri 33 na wahudumu wanne,” tume ya kuchunguza ajali hiyo ilisema.

Watu watano nao wanatibiwa hospitalini kutokana na majeraha ambayo walipata katika ajali hiyo.

Ndege hiyo ni ya kampuni ya Aeroflot ambayo ni ya kitaifa ya usafiri wa ndege na ililazimika kurejea kutua uwanjani baada ya kukumbwa na matatizo ya kiufundi.

Kufuatia ajali hiyo, ndege nyingine zilizotarajiwa kutumia uwanja huo zilielekezwa katika viwanja vingine vya ndege.

Ndege hiyo kwa jina Sukhoi Siperjet-100 ilipaa katika uwanja wa Sheremetyevo saa kumi na mbili jioni (saa za nchi hiyo) na ilikuwa ikielekea katika Jiji la Murmansk.

Wahudumu, hata hivyo, walitoa ilani kuhusu matatizo katika ndege muda mfupi tu baada ya kupaa.

Hata hivyo, punde tu baada ya kurejea uwanjani na kabla ya kumaliza kutua, injini za ndege zilishika moto ndege ilipokuwa kwenye barabara ya kutua ikaanza kuungua, kampuni ya Aeroflot ikasema kwenye ujumbe.

Kampuni hiyo ilisema kuwa wahudumu wa ndege “walifanya kila juhudi kuwaokoa wasafiri kwa sekunde 55.”

Kampuni ya Aeroflot ilichapisha orodha ya watu walioponea kifo, ikisema kuwa itaendelea kutoa habari zaidi jinsi zitakavyoendelea kuchipuka.

Kushika moto

Baadhi ya watu walidai kuwa injini za ndege hiyo zilishika moto baada ya kutua kwa kishindo na wala si ikiwa ingali hewani kama ilivyokuwa imeripotiwa awali, na kuwa ndege hiyo ilikuwa imejaribu kutua kwa mara ya kwanza lakini ikashindwa.

Kaimu Gavana wa Murmansk Andrey Chibis alisema kuwa familia za walioangamia katika ajali hiyo zitafidiwa Sh1.5 milioni, nao waathiriwa wanaotibiwa hospitalini wafidiwe Sh700,000.

Mikhail Savchenko alisema kuwa alikuwa katika ndege hiyo iliposhika moto, lakini akafanikiwa kuruka nje.

Mwanamume huyo, aidha alionyesha kanda ya video ikionyesha wasafiri wengine wakikimbia kutoka mahali ambapo ndege hiyo ilikuwa ikichomekea.

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameripotiwa kupewa habari za ajali hiyo na akatoa rambirambi zake kwa familia zilizoathirika, eneo hilo la Murmansk likitangaza siku tatu za maombolezo.