Kimataifa

Watu 756,000 katika hatari ya kufa njaa Sudan, UN yaonya

June 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

UMOJA WA MATAIFA, Amerika

KARIBU watu 756,000 nchini Sudan huenda wakakabiliwa na kero la ukosefu mkubwa wa chakula kufikia Septemba mwaka huu.

Hii ni kulingana na ripoti za uchunguzi ulioendeshwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa, pamoja na makundi ya kutoa misaada, utakaotumika kuamua iwapo hali hiyo inaweza kutangazwa kama janga la njaa.

Matokeo hayo ya awali, ya kufikia Juni 1, na yaliyoonekana na shirika la habari la Reuters, yanaonyesha kuwa, hali inaendelea kuwa mbaya zaidi Sudan, taifa linalozongwa na mapigano.

Ripoti ya hivi punde, iliyotolewa Desemba mwaka jana, ilionyesha kuwa, watu milioni 17.7 au asilimia 37 ya jumla ya idadi ya watu, wanakumbwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Lakini wakati huu inakadiriwa kuwa watu 25.6 milioni au asilimia 54 ya ujumla ya raia wa Sudan, wanakumbwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Idadi hiyo inajumuisha zaidi ya watu milioni tisa ambao wanahitaji msaada wa chakula kwa dharura.

Makisio ya sasa ni ya muda na yanaweza kubadilika.

Aidha, yatahitaji kuidhinishwa na serikali ya kijeshi ya Sudan, Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa.
Awali, serikali imekana ripoti kwamba, nchi hiyo inakabiliwa na ukosefu wa chakula.

Uchanganuzi huu mpya ulifanywa chini ya mwavuli wa mpango wa kukadiria hali ya uwepo wa chakula “Integrated Food Security Phase Classification (IPC).

Mpango huo ulianzishwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa, miungano ya kikanda na makundi ya kutoa misaada.

Mnamo Machi mwaka huu, IPC ilisema vitisho vya kiusalama, vizuizi barabarani na kuvurugwa kwa mawasiliano ya simu nchini Sudan vilikuwa vikitatiza uwezo wake wa kufanya ukaguzi.

IPC ambayo huchanganua data kuhusu hali ya utoshelevu wa chakula na utapiaji mlo, inatarajia kuchapisha ripoti kuhusu Sudan ndani ya wiki kadhaa zijazo, kulingana na watu wenye ufahamu kuhusu suala hilo.

Fatima Eltahir, afisa wa serikali ya Sudan ambaye pia ni mwenyekiti wa IPC nchini Sudan aliambia Reuters hivi: “Hatujamaliza. Matokeo ya mwisho hayajatolewa.”

Naye Lavonne Cloke, msemaji wa IPC, alisema uchanganuzi wa hali ya chakula Sudan unaendelea na haijulikani ni lini utakamilishwa.

Ukadiriaji wa hali nchini Sudan unajiri wakati kuna mapigano mengine katika Ukanda wa Gaza, ambapo hali ya ukosefu wa chakula inashuhudiwa.

Mnamo Machi mwaka huu, IPC ilisema jumla ya watu milioni 1.1, karibu nusu ya jumla ya watu Gaza, wanatarajiwa kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Nchini Sudan, mapigano yalilipuka katika jiji kuu Khartoum mnamo Aprili 2023 na yakaenea haraka katika sehemu zingine za nchi.

Aidha, mapigano hayo yalifufua mapigano ya kikabila katika eneo la Darfur, hali iliyolazimisha mamilioni ya watu kutoroka makwao.

Idadi ya watu waliotoroka makwao kutokana na mapigano ya sasa na yale ya zamani imepita milioni 10, kulingana na ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Uhamiaji (IOM).

Tayari Sudan inakabiliwa na changamoto kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa ulimwenguni ya watu kuhama makwao kutokana na vita.