• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Watu 99 wasafirishwa jongomeo na pombe haramu

Watu 99 wasafirishwa jongomeo na pombe haramu

AFP Na PETER MBURU

New Delhi, India

ANGALAU watu 99 waliaga dunia huku wengine wakikimbizwa hospitalini kaskazini mwa India baada ya kubugia pombe yenye sumu, serikali imetangaza.

Vifo hivyo vilitokea majimbo ya Uttar Pradesh na Uttarakhand, na habari kuvihusu zimekuwa zikiingia kwa siku tatu sasa, huku polisi wakishuku kuwa Methanol ilitumika kutengeneza pombe hiyo ya kifo.

Pombe ya bei rahisi na ya kutengenezwa kienyeji ni hali ya kawaida India, huku wagema wakishukiwa kuwa mara kwa mara huwa wanaongeza Methanol- aina fulani ya pombe ambayo si salama kwa matumizi ya binadamu, ili kuongeza nguvu ya kileo hicho.

Kunywa Methanol kwa wingi husababisha upofu, kuharibu ini na hata kifo.

Katika wilaya moja jumbo la Uttar Pradesh, watu 59 walikufa kwa kunywa pombe hiyo, msemaji wa polisi Shailendra Kumar, akaeleza AFP.

Afisa huyo wa polisi alisema kuwa katika wilaya jirani, watu tisa walifariki.

Hali hiyo ilisababisha polisi kuanzisha oparesheni kali dhidi ya wagema, ambapo 66 kati yao wanadaiwa kukamatwa. Sampuli za pombe walizokuwa nazo zilipelekwa kwa maabara kupimwa.

Polisi walisema angalau watu 31 walikufa katika jimbo jirani la Uttarakhand, ambapo wawili wengine walikamatwa kwa tuhuma za kusambaza pombe hiyo haramu.

Habari zaidi zilisema takriban watu 3,000 waliohusishwa na biashara hiyo haramu walikamatwa baada ya kisa hicho katika jimbo la Uttar Pradesh.

Kila mwaka, mamia ya watu masikini huaga dunia India kutokana na kunywa pombe yenye sumu, ya bei rahisi.

Mnamo 2015, zaidi ya watu 100 waliaga dunia Mumbai baada ya kunywa pombe haramu.

Kati ya lita bilioni tano za pombe ambayo hunywiwa India kila mwaka, takriban asilimia 40 huwa haramu.

  • Tags

You can share this post!

Amuua mumewe kwa sumu ili aolewe na mpenzi wake mfungwa

Aliyevunja nyumba avute bangi ashtuka kupata simba ndani

adminleo