• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
Watu watano wauawa katika fujo nchini Ivory Coast

Watu watano wauawa katika fujo nchini Ivory Coast

CHARLES WASONGA na AFP

ABIDJAN, Ivory Coast

WATU watano wameuawa huku wengine 100 wakijeruhiwa katika machafuko ya siku tatu yalishuhudiwa nchini Ivory Coast kupinga uamuzi wa Rais Alassane Ouattara kuwania urais muhula wa tatu, serikali ilisema Ijumaa.

Imewahimiza wananchi kudumisha utulivu huku walinda usalama wakiendelea kukabiliana na viongozi wa makundi ya waandamanaji.

Tangazo la Ouattara la kushiriki uchaguzi wa urais kwa mara nyingine liliibua kero miongoni mwa wakosoaji wake, kwani anaweza tu kuwania muhula wa tatu baada ya mageuzi ya Katiba.

Mapema Ijumaa, duru za usalama zilisema watu sita waliuawa katika ghasia hizo lakini Waziri wa Usalama Vagando Diamande baadaye alisema machafuko hayo yamesababisha vifo vya watu “watano huku wengine 104 wakijeruhiwa.”

Maafisa 10 wa polisi na mabawabu wawili ni miongoni mwa wale waliojeruhiwa.

Ouattara, 78, alitangaza wiki jana kwamba atashiriki tena uchaguzi wa urais ulioratibiwa kufanyika Oktoba 31.

Hatua hiyo ilijiri baada ya kifo cha Waziri Mkuu Amadou Gon Coulibaly ambaye alikuwa amemteua kuwa mrithi wake.

Jumla ya watu 68 wamekamatwa kwa kuchochea fujo na uharibifu wa mali ndani ya siku tatu za vurumai nchini humo, waziri Diomande alisema.

Mapema Ijumaa, polisi walisema mtu mmoja aliuawa katika mji wa Gagnoa, alikozaliwa Rais wa zamani Laurent Gbagbo.

“Mtu mmoja alifariki leo (Ijumaa) katika mapigano baina ya wanaounga mkono na wanaopinga uamuzi wa Rais Ouattara kuwania muhula wa tatu,” Meya wa Mji huo Yssouf Diabate aliambia AFP.

Uchaguzi huo wa Oktoba utafanyika wakati ambapo Ivory Coast ingali inapitia madhara yaliyosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotokea mnamo 2011 Gbagbo alipokataa kuondoka mamlakani baada ya Ouattara kumshinda uchaguzini.

Jumla ya watu 3,000 waliuawa na taifa hilo likagawanyika kuwili; kati ya maeneo ya Kaskazini na Kusini.

You can share this post!

UHALIFU: Watu wawili wauawa Samburu

Mwanariadha Joshua Cheptegei wa Uganda avunja rekodi ya...