Waziri Mkuu aliyejifungua akiwa ofisini achangamsha ulimwengu tena
MASHIRIKA na PETER MBURU
WAZIRI Mkuu wa New Zealand ambaye alichangamsha ulimwengu kwa kujifungua mtoto akiwa afisini Jumatatu alishangaza dunia tena, baada ya kumbeba mwanawe wa miezi mitatu hadi ukumbi wa makongamano wa UN.
Bi Jacinda Ardern ambaye ni wa umri wa miaka 38 alikuwa kiongozi wa pili wa dunia kujifunga akiwa afisini, wa kwanza akiwa Benazir Bhutto ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, ambaye alijifungua bintiye mnamo 1990.
Waziri huyo Mkuu alipigwa picha akimbusu na kumchezesha bintiye Neve katika ukumbi mkuu wa makongamano akiwa karibu na mpenzi wake Clarke Gayford walipokuwa katika mkutano uliopewa jina kongamano la amani la Nelson Mandela, ambapo aidha alihutubu.
Gayford, ambaye ni mtangazaji wa runinga moja alituma ujumbe Twitter wa picha ya kitambulisho cha binti yao cha kuhudhuria kongamano hilo ambacho kilisoma “mtoto wa rais wa New Zealand (New Zealand first baby).”
“Afadhali ningepata mtazamo wa mshangao wa maafisa kutoka Japan ndani ya chumba cha UN jana na kupata mtoto akibadilishwa mavazi. Itakuwa hadithi nzuri atakapofika miaka 21,” akaandika.
Ardern alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu Oktoba, miezi mitatu tu baada ya kuchukua uongozi wa chama cha Labour wakati kilikuwa katika hali mbaya kwa uchaguzi. Alirejea kazini mwezi uliopita baada ya kupumzika kwa wiki sita baada ya kujifungua.
Tayari alikuwa ametangaza kuwa wangesafiri kama familia kuelekea New York kwa makongamano ya UN ambapo alitarajiwa kuhutubu. Jumatatu alihutubu kuhusu masuala ya hali ya anga.