Kimataifa

Waziri Mkuu mpya wa Canada aitisha uchaguzi wa ghafla akilenga kuzima Trump

Na REUTERS, BENSON MATHEKA March 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Waziri Mkuu mpya wa Canada, Mark Carney, ametangaza uchaguzi wa dharura Aprili 28, akisema anahitaji mamlaka madhubuti kushughulikia tishio kutoka kwa Rais wa Amerika, Donald Trump, ambaye “anataka kutuvunja ili Amerika iweze kututawala.”

Uhusiano kati ya Amerika na Canada umedorora tangu Trump alipoanzisha ushuru na kutishia kufanya Canada jimbo  la Amerika. Ingawa uchaguzi ulikuwa umepangwa Oktoba 20, Carney anatumai kutumia kuimarika kwa umaarufu wa chama chake cha Liberal tangu Januari, baada ya Trump kuanza kuitishia Canada na Waziri Mkuu wa zamani Justin Trudeau kujiuzulu.

Baada ya kuapishwa Machi 14, Carney alisema anaweza kushirikiana na Trump, lakini sasa amechukua msimamo mkali zaidi. “Tunapitia mgogoro mkubwa zaidi wa maisha yetu kwa sababu ya hatua za biashara zisizo za haki za Trump na vitisho kwa uhuru wetu,” alisema baada ya Gavana Mkuu kuidhinisha uchaguzi huo.

Ikulu ya Amerika haikujibu mara moja kauli ya Carney. Mnamo Machi 6, Trump alichelewesha ushuru wa  asilimia 25 kwa bidhaa za Canada kwa siku 30, kabla ya kuweka ushuru kwa chuma  na kutishia ushuru zaidi Aprili 2.

“Kura za maoni zinaonyesha wasiwasi mkubwa wa Wacanada ni athari za sera za Trump,” alisema Nik Nanos wa shirika la utafiti la Nanos Research. Carney, ambaye hana uzoefu wa kisiasa, alishinda uongozi wa chama cha Liberal wiki mbili zilizopita kwa kudai kuwa ndiye mtu bora kumzima Trump.

Sasa ana wiki tano kuwashawishi wapiga kura. Jumapili, alipendekeza kupunguza kiwango cha chini cha kodi ya mapato kwa asilimia moja. Kura za maoni zinaonyesha chama cha Liberal sasa kiko mbele kidogo ya Conservative kwa umaarufu.

Chama cha Conservative kinamshutumu Carney kwa kuendeleza sera za matumizi makubwa za Trudeau na kutokuwa wazi kuhusu mali yake ya kifedha. Carney alijibu kwa hasira alipohojiwa kuhusu mfuko wake wa uaminifu, jambo linaloweza kumpa matatizo kwenye kampeni yake.

Ushindi wake utategemea kura za jimbo la Quebec, ambako alipata shida kujibu kwa Kifaransa katika mkutano wa waandishi wa habari. Pierre Poilievre, kiongozi wa Conservatives, ana uzoefu mkubwa wa kisiasa na anazungumza Kifaransa kwa ufasaha.

Utafiti wa Angus Reid uliweka umaarufu wa Liberals kuwa 42 na Conservatives asilimia 37. Profesa Laura Stephenson alisema athari ya Trump inaweza kumpa Carney unafuu usio wa kawaida kwa mgombea asiye na uzoefu wa kisiasa.