Kimataifa

Waziri Mkuu wa zamani atekwa nyara nchini Chad

Na MASHIRIKA May 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Waziri Mkuu wa Chad Succes Masra alitekwa nyara na maafisa wa usalama nyumbani kwake Ijumaa iliyopita, chama chake kimesema.

Masra ambaye pia ni kiongozi wa upinzani, amekuwa mwiba kwa serikali ya Rais Mahamat Idriss Derby. Babake Mahamat, Rais Idriss Derby aliuawa mnamo 2021 alipokuwa akitembelea vikosi vya serikali vilivyokuwa vikipambana na wapiganaji kaskazini mwa nchi hiyo.

Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Transformers Ndolembai Sade Njesada alitoa kanda ya CCTV ikionyesha kwamba maafisa wa usalama waliojihami wakiondoka na Masri katika makazi yake rasmi. Serikali bado haijasema chochote kuhusu tukio hilo.

Masra aliteuliwa waziri mkuu mnamo Januari 2024 kwa lengo la kufurahisha upinzani, miezi minne baada ya uchaguzi ambao Mahamat alikuwa ameshinda kwa asilimia 61 za kura.  Kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya urais, Masra alikuwa amedai ndiye alikuwa mshindi na akasema kulikuwa na udanganyifu kwenye uchaguzi huo.

Alijiuzulu kama waziri mkuu kabla ya Mahamat kuapishwa. Chad ilikuwa nchi ya kwanza kuandaa uchaguzi kati ya mataifa ya magharibi na kati mwa Afrika yaliyokuwa yamepitia mapinduzi ya kijeshi na misukosuko ya uongozi.

Kutekwa nyara kwa Masra kunaonyesha jinsi ambavyo demokrasia inaendelea kukandamizwa na utawala cha Chad ambapo hata vyombo vya habari vimekuwa vikidhibitiwa.