Waziri wa masuala ya umaskini afutwa kwa kujiwekea Sh96 milioni akaunti ya kibinafsi
Na MASHIRIKA
Rais wa Nigeria amemsimamisha kazi waziri mmoja kwa kujiwekea Sh96 milioni za walipa ushuru kwenye akaunti ya kibinafsi.
Waziri wa Masuala ya Uhisani na Ukabilianaji wa Umaskini Betta Edu alisimamishwa kazi Jumatatu, Januari 8, 2024 kufuatia malumbano makali kutoka kwa umma kuhusiana na sakata hiyo.
Taarifa iliyotoka kwa Rais Bola Tinubu ilisema uchunguzi umeanzishwa kubaini ufujaji huo katika wizara ya Dkt Edu.
Hata hivyo, waziri huyo amekanusha kufanya kosa lolote.
Afisi yake ilisema kwamba aliidhinisha kuwekwa kwa pesa hizo kwenye akaunti ya kibinafsi, ila haikuwa kwa jina lake, bali akaeleza kwamba pesa hizo ni za “kugawa kwa makundi yanayokabiliwa na changamoto nyingi”.
Dkt Edu, aliye na umri wa miaka 37, ndiye waziri mchanga zaidi katika serikali ya Rais Tinubu na huonekana kama mwandani wa karibu wa rais huyo.
Kusimamishwa kazi ni jambo nadra mno nchini Nigeria, na Dkt Edu ndiye wa kwanza kufutwa tangu Rais Tinubu alipochukua hatamu za uongozi mnamo Mei 2023.
Mtangulizi wa Tinubu, Muhammadu Buhari alifuta kazi mawaziri wawili pekee katika miaka yake minane ya uongozi.
Wiki jana, vyombo vya habari nchini humo viliripoti stakabadhi ‘iliyovujishwa’ ambayo inadaiwa kuonyesha Dkt Edu akimwelekeza afisa wa ngazi za juu katika Wizara ya Fedha kutuma pesa hizo kwa akaunti ya kibinafsi ya Bridget Oniyelu, ambaye ni mhasibu wa mradi wa Hazina ya Makundi ya Wasiojiweza.
Ripoti kwamba Dkt Edu aliagiza pesa hizo ziwekwe kwenye akaunti ya kibinafsi na sio ya kiserikali ilizua ghadhabu miongoni mwa umma wa Nigeria.
Bw Tinubu ameagiza uchunguzi ufanywe kuhusiana na kisa hicho cha Jumapili.
Ameitaka Tume ya Kupambana na Makosa ya Kiuchumi na Kifedha (EFCC) kufanya “Uchunguzi wa kina kuhusu hali zote za matumizi ya fedha katika wizara ya Dkt Edu” na kuchukua hatua zifaazo.
- Imetafsiriwa na FATUMA BARIKI