Kimataifa

Waziri wa Ulinzi wa Amerika alazwa tena hospitalini kwa tatizo la kibofu

February 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MASHIRIKA

WAZIRI wa Ulinzi wa Amerika, Lloyd Austin, alilazwa hospitalini mjini Washington Jumapili kwa matibabu ya “dalili zinazoashiria tatizo la kibofu”, msemaji wa Pentagon alisema.

Austin, 70, baadaye alikabidhi majukumu ya ofisi yake kwa Naibu Waziri wa Ulinzi ,Kathleen Hicks, Katibu wa Habari Pentagon Meja Jenerali Pat Ryder alisema katika taarifa.

Wabunge wa Republican na Democratic walikosoa Austin kwa kukosa kufichua anaugua saratani baada ya kulazwa hospitalini mnamo Desemba na Januari.

Baadhi ya Wanarepublican mashuhuri akiwemo Rais wa zamani Donald Trump walitaka Austin aondolewe kazini.

Wakati huo huo, jeshi la Amerika lilisema Jumapili kwamba lilishambulia maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi nchini Yemen na kuharibu makombora ambayo yalikuwa yakiandaliwa kurushiwa meli katika Bahari ya Sham.

Mashambulizi hayo yalifanyika Jumamosi kaskazini mwa mji wa Hodeida, Msemaji wa Jeshi wa Amerika, alisema kwenye mtandao wa kijamii.

Jeshi la Amerika “lilitekeleza mashambulizi na kuharibu kwa mafanikio makombora matatu ya kushambulia meli iliyokuwa ikiandaliwa kurushiwa meli katika Bahari ya Sham,” taarifa ya jeshi ilisema.

Kituo cha televisheni cha Wahouthi, Al-Masirah Jumamosi usiku kiliripoti mashambulizi matatu kwenye eneo la bandari ya Salif.

Mashambulizi hayo ni sehemu ya hatua zilizochukuliwa na Amerika na washirika wake dhidi ya waasi wa Wahouthi.