WHO yataja virusi vya China janga maambukizi yakienea
Na MASHIRIKA
CHINA mnamo Ijumaa ilitangaza kuwa itatuma ndege kote ulimwenguni kuchukua raia wote wanaotoka jiji la Wuhan ambako virusi vya homa kali ya Coronavirus vilianzia huku mataifa yakisimamisha safari za ndege kwenda nchi hiyo.
Haya yanajiri huku Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), likikiri kuwa maradhi hayo ni suala la dharura kimataifa na idadi ya waliofariki nchini China ikifika 259 nayo idadio ya maambukizi ikiwa 11,791 katika taifa hilo na idadi jumla ya visa vya Corona ikifikia watu 11,943 kote duniani.
China imeshauri raia wake kuahirisha safari za kwenda ng’ambo na ikafuta safari za vikundi vya watalii huku nchi kadhaa kama vile Amerika, Ujerumani, Uingereza na Japan zikiwaonya raia wake kutozuru nchi hiyo.
“Kufuatia changamoto na hali ngumu ambayo raia wa China kutoka mkoa wa Hubei na hasa Wuhan wamepitia ng’ambo, serikali ya China imeamua kutuma ndege za kukodisha kuwachukua na kuwasafirisha moja kwa moja hadi Wuhan, haraka iwezekanavyo,” wizara ya mashauri ya kigeni ilisema kupitia msemaji wake Hua Chunying.
Wuhan, ambako maafisa wa serikali walisema virusi hivyo vilianzia katika soko la wanyama ni miongoni mwa miji 15 iliyotengwa katika juhudi za kuzuia kuenea kwa homa hiyo hatari na isiyo na tiba.
Hatua ya China ya kuwarejesha raia wake Wuhan ilijadiliwa mno kwenye mitandao ya kijamii baadhi ya watu wakihoji kuwa huenda raia hao wakatae kurudi.
Alipoulizwa kuhusu hatua ya mashirika ya ndege ya kimataifa ya kusimamisha safari za ndege, Zhu Tao, afisa wa Mamlaka ya Safari za ndege ya China alisema serikali ina jukumu la kurejesha raia wake nyumbani.
Hospitali katika mji huo zina idadi kubwa ya wagonjwa. Wanahabari wa AFP walisema waliona milolongo mirefu katika hospitali, baadhi ya wagonjwa wakisema wamekuwa wakisubiri kwa siku mbili kabla ya kumuona daktari.
Kuna hofu kuwa huenda raia wa China walio mataifa ya ng’ambo wakaanza kubaguliwa kufuatia kuenea kwa maradhi hayo hadi zaidi ya mataifa 20 kote ulimwenguni. Mfano mzuri ni Mongolia.
WHO ilisema ilitangaza maradhi hayo kama janga la kimataifa baada ya kuenea nje ya China.
“Sababu kuu ya kutoa tangazo hilo sio kile kinachoendelea China lakini kinachotendeka katika mataifa mengine,” alisema mkurugenzi mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Alisema wasiwasi wa shirika hilo ni kuwa, huenda maradhi hayo yakaenea hadi mataifa yasiyo na uwezo wa kuyakabili.
Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa, watu 98 wamepata virusi hivyo katika mataifa mengine 18 kote ulimwenguni. Hakuna aliyefariki katika mataifa hayo.