Kimataifa

Yaibuka wanawake wanalazimishiwa ngono ili wapate chanjo dhidi ya Ebola

June 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA MASHIRIKA

WANAWAKE wanashurutishwa kufanya ngono katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ili wapewe dawa za kujikinga kutokana na ugonjwa wa Ebola, madai yameibuka.

Hofu kuwa wafanyakazi walioaminiwa kutoa chanjo za ugonjwa huo wananyanyasa wanawake imezidi, ikidaiwa kuwa sasa inawabidi wanawake kukubali kulala nao kwa woga wa kupata ugonjwa huo.

Ripoti hizi zinakuja wakati vifo vinavyotokana na mkurupuko wa Ebola vimefikia zaidi ya watu 500. Ripoti hizo aidha zimeibuka siku chache tu baada ya wizara ya afya nchi hiyo kutangaza kuwa chanjo hizo zimesaidia maelfu ya watu kuepuka kifo kutokana na ugonjwa wa Ebola.

Kikundi cha watu waliohojiwa na Mashirika walieleza kuwa baadhi ya wafanyakazi wanawataka kulala nao ili wapewe tiba za Ebola, zikiwemo chanjo ya kujizuia kutokana na ugonjwa huo.

Uchunguzi uliofanywa na Mashirika Yasiyo ya Serikali ulionyesha kuwa kuna ukosefu wa uaminifu miongoni mwa wafanyakazi katika sekta ya afya nchi hiyo.

Jumamosi, maafisa wa serikali walitangaza kuwa zaidi ya watu 500 wamefariki kufuatia mkurupuko wa hivi punde zaidi wa ugonjwa wa Ebola, lakini utoaji chanjo ukazuia maelfu ya watu kutoangamia.

“Kwa jumla kumekuwa na vifo 502 na watu wengine 271 waliotibiwa,” ripoti ya wizara ya afya ikasema.

Waziri wa afya Oly Ilunga Kalenga alisema kwa mara ya kwanza chanjo hizo zimelinda watu 76, 425 na kuzuia maelfu wengine kutokana na kifo.

“Naamizi tumezuia kuenea kwa ugonjwa huu katika miji mikubwa eneo hili,” akasema waziri huyo.

Mkurupuko wa ugonjwa huo ulianza Agosti katika eneo la kaskazini mwa taifa hilo, Kivu, ambalo linapakana na Uganda na Rwanda.