Kimataifa

Zaidi ya watu 1000 Sudan wameuawa na RSF – UN

Na MASHIRIKA, WINNIE ONYANDO December 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WANAMGAMBO wa kikosi cha RSF ambao wamekuwa wakipambana na jeshi la serikali kwa muda wa miaka miwili na nusu, walisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000 wakati wa mashambulio ya siku tatu yaliyofanywa mwezi Aprili.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Desemba 18, 2025.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu OHCHR imeeleza katika ripoti yake kwamba “ilirekodi mauaji ya raia 1,013 wakati wa mashambulio ya RSF kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam kati ya Aprili 11 na 13.”

Ripoti hiyo imeongeza kuwa zaidi ya wakimbizi 400,000 waliokuwepo kwenye kambi hiyo walilazimika kukimbia wakati wa mashambulio hayo ya siku tatu.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, mapigano kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa RSF yamesababisha takriban watu milioni 12 kuyahama makazi yao nchini Sudan huku maelfu wakikabiliwa na njaa.