Kimataifa

Zuma sasa huru kuwania urais licha ya hukumu ya uhalifu

April 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

PRETORIA, AFRIKA KUSINI

NA MASHIRIKA

RAIS wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma yuko huru kugombea katika uchaguzi mkuu wa mwezi Mei baada ya mahakama kubatilisha marufuku aliyowekewa.

Mwezi uliopita tume ya uchaguzi ilimzuia kuwania kiti hicho kwa kudharau hukumu ya mahakama.

Tume hiyo ilisema kuwa katiba inazuia watu kushikilia ofisi ya umma ikiwa watapatikana na hatia ya uhalifu na kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi 12 gerezani.

Bw Zuma, 81, amekuwa akifanya kampeni chini ya chama kipya cha Umkhonto we Sizwe (MK).

Kigogo huyo wa zamani wa chama tawala cha African National Congress (ANC), ni mtu mwenye utata na aliwahi kuwa rais kuanzia 2009 hadi 2018, alipolazimika kung’atuka kwa tuhuma za ufisadi.

Alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela mwaka wa 2021 kwa kukosa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa ufisadi, ingawa alitumikia miezi mitatu tu kwa sababu ya masuala ya kiafya.

Uamuzi huo unaweza kuwa na athari kubwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mwezi ujao.

Sura ya chama kipya cha upinzani

Bw Zuma ni sura ya chama kipya cha upinzani cha MK, ambacho kimepewa jina la tawi la zamani la kijeshi la ANC.

Rais huyo wa zamani anajiona kama mrithi wa kweli wa mizizi ya mapinduzi ya ANC, iliyowahi kuongozwa na Nelson Mandela.

Ushindi wa Bw Zuma katika mahakama unamaanisha kuwa sasa anaweza kuwania kiti hicho kama mgombea mkuu wa MK.

Badala ya kumpigia kura rais moja kwa moja, Waafrika Kusini huchagua wajumbe wa Bunge la Kitaifa. Baadaye, wajumbe humchagua kiongozi mkuu wa nchi.

Uamuzi huo pia utakuwa pigo kwa ANC, ambayo baada ya miaka 30 madarakani, inakabiliwa na dosari kadhaa.

Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa enzi ya kidemokrasia mwaka 1994, idadi ya kura za ANC inaweza kushuka chini ya asilimia 50, kura nyingi za maoni zinatabiri.

Jumatatu, Zuma mwenye umri wa miaka 81 alikuwa mahakamani mjini Johannesburg wakati mawakili wakijadi kesi hiyo.

“Ikiwa raia wanataka niwe rais, nani atawazuia,” Zuma aliwambia wafuasi wake baada ya kesi kusikilizwa. “Niruhusu niende na nimalizie kile nilichokianza.”

Afrika Kusini itakuwa na uchaguzi mkuu tarehe Mei 29 ambao unatarajiwa kuwa uchaguzi wenye ushindani mkali tangu ujio wa demokrasia mwaka 1994.

Chama tawala cha African National Congress kinakabiliwa na changamoto katika kura ya maoni na kuna hatari kuwa kitapoteza idadi kubwa ya wabunge kutokana na kudorora kwa uchumi na madai ya ufisadi na usimamizi mbaya.