HabariSiasa

Kinaya Kenya ikiwapa Wachina mkopo wa mabilioni bila riba

June 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LEONARD ONYANGO

Uchina ilipunja Kenya katika mchakato wa kutia saini mkataba wa Sh324.01 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mombasa hadi Nairobi.

Kulingana na stakabadhi zilizoonekana na Taifa Leo Dijitali, Uchina ndiyo ilirudi kunufaika na mkopo huo huku Kenya ikiambulia patupu.

Kwa mfano, baada ya kukamilisha ujenzi wa SGR, kampuni ya China Roads and Bridges Corporation (CRBC) inayoendesha treni, ilichukua mkopo wa Sh3.5 bilioni kutoka kwa Shirika la Reli la Kenya.

CRBC ilichukua mkopo bila riba kuendeshea shughuli za reli mpya.

Katika mkataba wa siri, si lazima Uchina irudishe hela hizo zikiwa taslimu.

Shirika la Reli la Kenya pia liliipa CRBC Sh3 bilioni zaidi kuhakikisha kwamba akaunti ya kuendeshea treni ina fedha za kutosha.

Kenya ilipatia Wachina hela zingine Sh1.3 bilioni kuwezesha maafisa wa CRBC kuzoea mazingira mapya.

Kampuni ya CRBC inalipwa ada ya kuendesha treni za SGR hata kama mradi huo unapata hasara. Hiyo inamaanisha kwamba hata treni zisipofanya kazi bado Kenya italipa Uchina fedha za kuendeshea mradi huo.

Kenya inatoa fedha za kutengeneza treni zinapoharibika, Uchina haitatoa hela zozote. Kenya ni miongoni mwa mataifa yaliyo na deni kubwa zaidi la China barani Afrika.

Data za Wizara ya Fedha zinaonyesha kuwa kenya inadaiwa zaidi ya Sh800 bilioni na Uchina.

Ripoti iliyotolewa na shirika la Amerika, Centre for Global Development ilisema kuwa Uchina imekopesha mataifa ya Afrika zaidi ya Sh1.4 trilioni.

Ripoti ya Wizara ya Fedha inaonyesha kuwa kwa kila mkopo wa Sh100 ambao Kenya ilitia saini na mataifa ya Kigeni, Sh70 zinatoka China.

Mbali na Kenya, mataifa mengine barani Afrika ambayo yamelemewa na mzigo wa madeni ya China ni Angola (Sh4.28 trilioni) na Ethiopia (Sh1.37 trilioni).