Kingi aungama PAA ina kibarua kutikisa ushawishi wa ODM serikalini
SPIKA wa Seneti, Bw Amason Kingi, ameungama kuwa siri ya nguvu za chama cha kisiasa ni idadi ya wabunge.
Bw Kingi, ambaye chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA) kilipata viti vitatu bungeni 2022, amerai Wapwani kukiunga mkono 2027.
Gavana huyo wa zamani wa Kilifi alisema kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, amepata ushawishi mkubwa ndani ya serikali ya Rais William Ruto, kwa sababu ana wabunge wengi chamani.
“Sahizi Raila akipiga tu simu moja, maendeleo yatamiminika huko Nyanza, lakini mimi Kingi sina sauti kwa sababu sina wabunge kwa hivyo ninawarai tutembee pamoja 2027,” akasema, baada ya kuzindua maabara katika Shule ya Upili ya Bang’a iliyo Kinango, Kaunti ya Kwale.
“Mwaka wa 2027, pelekeni sauti kubwa na ya kutisha kule bunge na tuone vile maendeleo yatakavyomiminika Pwani hii,” akaongeza.
Bw Kingi aliunda PAA miezi michache kabla Uchaguzi Mkuu wa 2022, alipokuwa amehama ODM. Lengo lake lilikuwa kufanya chama hicho kiwe cha kutetea maslahi ya Wapwani lakini akatengwa na wanasiasa wengi wa ukanda huo.