Habari

Kinuthia Mbugua ashutumiwa kwa kufeli kufika mbele ya PAC

February 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MSIMAMIZI wa Ikulu Kinuthia Mbugua ametakiwa kufika mbele ya wabunge Jumatatu wiki ujao kujibu maswali yaliyoibuliwa na Mhasibu Mkuu wa Serikali Edward Ouko kuhusiana na matumizi ya fedha za umma katika Afisi ya Rais.

Hii ni baada ya ripoti kuhusu matumizi ya fedha katika mwaka wa kifedha wa 2015/2016 kubaini visa vya wizi au ubadhirifu wa pesa za umma katika Afisi ya Rais.

Bw Mbugua alikuwa akitarajiwa kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu uhasibu kujibu maswali hayo Alhamisi lakini akafeli.

Badala yake alituma barua kupitia afisi ya Karani wa Bunge Michael Sialai akiomba atengewe siku nyingine kwa sababu alikuwa amebanwa na shughuli nyingi katika Ikulu.

Hata hivyo, mwenyekiti wa PAC Opiyo Wandayi alimkosoa Bw Mbugua akisema majukumu ya kamati hiyo yana uzito mkubwa zaidi kuliko majukumu mengine ya kila siku ya maafisa wa serikali wanaohitajika kufika mbele yake.

Siri

Bw Mbugua anahitajika kutoa mwanga kuhusu Sh2.7 bilioni, zilizotajwa kama ‘matumizi ya kisiri’ katika Ikulu ya Rais, zilivyotumika kati ya mwaka wa 2013 na 2016.

Katika ripoti yake ya ukaguzi Bw Ouko anasema kuwa japo Afisi ya Rais iliwasilisha stakabadhi za kuonyesha jinsi pesa zilivyotumika, masuala kuhusu matumizi hayo ya kisiri bado hayajafafanuliwa kwa ukamilifu.

Masuala yaliyobainishwa na Mhasibu Mkuu ni  kama vile, malipo kwa bidhaa ambazo hazikuwasilishwa, malipo tata kwa magari na madeni ambayo hayajalipwa na Afisi ya Rais kuanzia 2013 hadi 2016