Habari

Kioja, Kioni akikataa kushiriki mjadala wa TV na Maalim aliyedaiwa kupendekeza mauaji ya Gen Z

Na CHARLES WASONGA October 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KIOJA kilishuhudiwa katika studio za runinga moja ya humu nchini Jumatano Oktoba 23, 2024 baada ya Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni kukurupuka nje baada ya kugundua angeshiriki mjadala na Mbunge wa Dadaab Farah Maalim.

Alisema hawezi kuketi pamoja na Bw Maalim baada ya Mbunge huyo wa Wiper kudai, miezi miwili iliyopita, kuwa laiti angalikuwa rais angeamuru kuuawa kwa vijana 500o wa Gen-Z waliozua vurugu nchini Juni kupitia maandamano ya kupinga Rais William Ruto

Bw Kioni, ambaye ni Mbunge wa zamani wa Ndaragua, alikuwa amealikwa katika studio za runinga ya TV 47 kujadili masuala yanayoathiri taifa saa za asubuhi.

Lakini hakuwa na habari kwamba angeshiriki mjadala huo pamoja Bw Maalim ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Wiper.

“Endelea tu, siwezi kuketi pamoja na mtu kama huyo,” Kioni akasema huku akifunganya virago vyake kuondoka.

Baadaya kuondoka, kinara huyo wa Azimio alieleza kuwa alikerwa zaidi na uamuzi wa serikali wa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya Gen-Z, wengi wao wakikamatwa na wengine zaidi ya 60 wakiuawa.

“Siwezi kuketi kufanya majadiliano na Farah Maalim aliyependekeza mauaji ya Gen-Zs 5000 nchini. Taifa hili linaangamia kwa sababu ya watu wasio na moyo wa ubinadamu, tunaowaita viongozi wa kitaifa. Siwezi kushusha hadhi yangu kwa kushiriki mjadala na viongozi kama hao,” Bw Kioni akaeleza.

Mnamo Julai 11, mwaka huu, Tume ya Uwiano wa Kitaifa na Utangamano (NCIC) ilimwagiza Bw Maalim kufika mbele yake kuhusiana na madai hayo yaliyofasiriwa kama ya uchochezi.

Kwenye taarifa Jumatano tume hiyo inayoongozwa na Kasisi Samuel Kobia ilisema ilianzisha uchunguzi kuhusiana na kauli ya mbunge huyo kwamba “ningekuwa rais ningeamuru kuchinjwa kwa Gen-Zs wote waliotekeleza kitendo cha uhaini kwa kuvamia majengo ya bunge Juni 25, 2024.”

Hata hivyo, Bw Maalim, ambaye ni Naibu Spika wa zamani katika Bunge la Kitaifa, alikana kutoa madai hayo akisema “nilieleweka vibaya.”