Habari

Kitendawili cha maiti kusalia mochari kwa miaka 15

September 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na STEPHEN MUTHINI

MWILI wa mwanamume kutoka kijijini Ndelekeni, eneobunge la Masinga, Kaunti ya Machakos umekwama mochari kwa miaka 15 sasa baada ya mkewe kuukataa akidai kwamba mume wake angali hai na atarejea nyumbani siku moja.

Stephen Nthuku alifariki dunia miaka 15 iliyopita baada ya kuuawa katika hali ya kutatanisha nyumbani kwake.

Nthuku alikuwa akiishi jijini Mombasa ambapo alifanya kibarua kama njia ya kujipa riziki. Aliporejea nyumbani Desemba 2003 alipata mkewe, Stellamaris Nthuku, akiwa na mwanamume mwingine nyumbani kwake.

Kwa kuwa mpango huo wa kando, Mutunga Kyongo, alikuwa mtu wa miraba minne, Nthuku aliondoka na kwenda kulala kwa ndugu yake.

Kesho yake Nthuku alielezea jamaa zake aliyoyaona na wakamshauri akaripoti kwa baraza la wazee wa ukoo wa Amutei.

Wazee waliandamana hadi nyumbani kwa Nthuku kwenda kumtakasa.

Lakini walipofika, Stellamaris alitangaza kuwa Kyongo ndiye mumewe na kuanza kuwafanyia vioja vya kutisha. Katika kilele cha vioja, Stellamaris alivua nguo na kuanza kuwalaani kwa chupi yake aliyoitia maji. Wazee wakatimua mbio.

Vituko hivyo vimeorodheshwa katika ushahidi uliokuwa umetolewa kortini ambao Nthuku alitoa akitaka watalikiane na mkewe.

Lakini kabla ya talaka hiyo kukamilika, Nthuku aliuawa katika hali ya kutatanisha na kuanzia wakati huo imesalia kuwa kesi mahakamani. Maiti ya Nthuku imehifadhiwa katika mochari ya City jijini Nairobi.

Ushahidi uliotolewa na dada wa Nthuku, Bi Mbisu King’ele pamoja na mashahidi wengine wanane, ulielezea namna Stellamaris alivyomhadaa Nthuku kuingia ndani ya nyumba ambapo walimshambuliwa na mpenzi wake Kyongo.

Walidai kwamba mwendazake alipigwa kwa kifaa butu kichwani na mwili wake kutupwa chooni. Baadaye walikodisha mkokoteni na kutupa maiti hiyo katika msitu wa B2 Yatta.

Mwanakemia wa serikali alishindwa kubaini ikiwa mwili huo ulikuwa kweli wa Nthuku kwani alisema kuwa mifupa ya mwendazake iliyoko katika mochari ya City haikutoa matokeo sahihi ya DNA.

Stellamaris ambaye sasa anakabiliwa na kesi ya mauaji, alisisitiza kuwa maiti hiyo si ya mumewe huku akisema kwamba ana matumaini mume wake atarejea nyumbani siku moja.

Mashahidi wote wamefariki isipokuwa mtoto anayedaiwa kuona maiti ya mwendazake ikiwa chooni.

Mtoto huyo alitoweka kwa miaka kadhaa na aliporejea alikuwa amebadili ushahidi alioutoa hapo awali.

Polisi wameshikilia kuwa mazishi hayatafanyika hadi pale maiti hiyo itakapotambuliwa.