Habari

Kiu kuzidi Pwani mradi wa Mzima ukikwama

January 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LUCY MKANYIKA

WAKAZI wa Pwani watalazimika kusubiri kwa muda mrefu kutekelezwa kwa mradi wa bomba la pili la Mzima kutokana na uhaba wa pesa.

Mradi huo ambao ungegharimu serikali Sh42 bilioni haujang’oa nanga miaka miwili baada ya serikali kutoa ahadi ya kuuanzisha.

Bomba hilo linatarajiwa kusambaza maji kwa kaunti nne za Pwani, ambazo ni Taita-Taveta, Kwale, Kilifi na Mombasa.

Chemichemi za Mzima hutoa mamilioni ya lita za maji kila siku, lakini bomba la kwanza lililojengwa 1957 halitoshelezi mahitaji ya wakazi wa Pwani.

Akiongea alipozuru chemichemi hiyo iliyoko katika Mbuga ya Tsavo Magharibi, mwenyekiti wa Bodi ya Maji katika eneo la Pwani, Bw Mustafa Idd, alisema kuwa tayari wamefanya utafiti kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Bw Iddi alisema kuwa mradi huo utaanza punde tu fedha zitakapopatikana.

“Tutahakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa mara moja ili kuhakikisha wenyeji wa Pwani wanapata maji ya matumizi. Ni wajibu wetu hukakikisha kuwa tunamaliza shida ya uhaba wa maji katika eneo hili,” akasema.

Waziri wa Maji wa Kaunti ya Taita-Taveta, Bw Gasper Kabaka, alisema kuwa serikali hiyo iko tayari kushirikiana na bodi kutunza chemichemi ya Mzima.

Bw Kabaka alisema kuwa mradi huo wa bomba la pili utamaliza uhaba wa maji unaotatiza wenyeji wa kaunti hiyo.

Mradi huo ulikuwa ahadi ya serikali ya Jubilee kwa wakazi wa Pwani wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2017.

Mwaka 2019 Seneta Jones Mwaruma alidai kuwa serikali iliwahadaa Wapwani kwani hakuna pesa zilizotengwa kuutekeleza.