Habari

Kiunjuri atetea hatua ya serikali kununua mahindi kutoka nje

June 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Kilimo Mwangi Kiunjuri ametetea hatua ya serikali kuagiza mahindi kutoka mataifa ya kigeni.

Kulingana na waziri, mahindi yanayovunwa nchini kila mwaka hayatoshi kukimu Wakenya.

“Kwa mwaka Kenya huvuna karibu magunia milioni 44 ya mahindi, idadi hii haitoshi kulisha Wakenya,” amesema Bw Kiunjuri kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Inooro FM.

Kauli yake imejiri kufuatia tahadhari kuwa huenda taifa likakumbwa na njaa hivi karibuni kwa sababu ya kiangazi kilichoshuhudiwa mapema mwaka 2019.

Mvua ya masika ambayo kwa kawaida hapa nchini imekuwa ikishuhudiwa Machi ilichelewa mwaka huu wa 2019.

Waziri amesema Kenya imetia mkataba na baadhi ya mataifa ya kigeni kununua mahindi wakati mazao yanayovunwa nchini hayatoshi hasa msimu wa njaa.

“Kenya imetia mkataba na mataifa ya kigeni yanayokuza mahindi. Upungufu wa nafaka hii unapotokea kwa mwaka taifa linaruhusiwa kuagiza magunia milioni 12,” alisema.

Waziri amesema wiki ijayo magunia 2 milioni yatatolewa kutoka mabohari ya serikali ili kukabiliana na upungufu wa unga wa mahindi uliopo.

Alionya kuwa endapo serikali haitanunua mahindi kutoka nje, bei ya unga huenda ikafikia Sh125.

“Tusipofanya hivyo, bei ya unga itapanda na hakuna Mkenya atakubali kuununua kwa bei ghali,” amesema.

Pakiti ya kilo mbili kwa sasa inauzwa kwa bei ya zaidi ya Sh110.

Amjesema gunia moja la kilo 90 litanunuliwa kwa kati ya Sh3,000 na Sh3,400.

Amefafanua kwamba kwa wakulima wenye mahindi nchini pia bei itakuwa ni iyo hiyo.

Mazao ya kutosha

Eneo la North Rift ndilo hukuza mahindi kwa wingi, na baadhi ya viongozi humo wanakosoa hatua ya serikali kuagiza mahindi kutoka nje wakisema taifa lina mazao ya kutosha.

“Maghala ya wakulima mahindi yanaendelea kuoza na mengine kushambuliwa na wadudu. Serikali hununua mahindi ya wakulima kwa bei ya chini na ndio maana wanakataa kuyauza,” anasema mbunge mwakilishi wa wanawake Uasin Gishu Gladys Boss Shollei.

Mwaka uliopita, msimu wa mavuno ya 2018/2019 serikali iliidhinisha wakulima kulipwa Sh2,300 gunia la 90 kupitia bodi ya mazao na nafaka (NCPB). Ni hatua ambayo ilizua tumbojoto kati ya wakulima, baadhi viongozi kutoka Bonde la Ufa haswa yanayozalisha mahindi na serikali.

Wakulima wakiungwa mkono na viongozi hao waliitaka serikali kununua gunia moja kwa Sh3, 200. Wakulima walihoji wanaendelea kukadiria hasara ikizingatiwa gharama ya pembejeo imepanda.

Hata hivyo, serikali ilipuuza ombi la wakulima hao ikihoji haina fedha za kutosha kununua mazao walivyotaka.