Habari

Kizaazaa polisi kufurika kortini kuokoa mwenzao aliyetupwa seli

November 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na TITUS OMINDE na SETH MOIBEN

KIZAAZAA kilishuhudiwa katika mahakama ya Eldoret maafisa wakuu wa polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu, walipofurika kortini kujaribu kumshawishi hakimu amwachilie mmoja wao aliyezuiliwa kwa kukosa kuheshimu agizo la mahakama.

Maafisa wapatao 10, wakiongozwa na kamanda wa polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu, Johnstone Ipara, walifika mahakamani ili kujaribu kumtetea mwenzao.

Hakimu mkuu wa mahakama ya Eldoret, Linus Kaissan, aliamuru Bw Solomon Wamai ambaye anasimamia kituo cha polisi cha Eldoret Magharibi azuiliwe seli kwa kukosa kufuata agizo la mahakama kufikisha washukiwa wawili kortini.

Washukiwa hao walikamatwa kwa madai ya kupatikana na katoni zaidi ya 200 za sigara zilizoingizwa nchini kinyume cha sheria.

Wakili wa washukiwa hao alipata agizo lililomtaka afisa huyo kuwafikisha washukiwa hao mahakamani Alhamisi.

Korti hiyo ilitoa amri Bw Wamai afike mahakamani kuelezea kwa nini alikosa kuwafikisha washukiwa hao alivyoagizwa.

Alipofika kortini, afisa huyo alikubali kwamba alikuwa amepokea agizo la mahakama kutoka kwa wakili wa washukiwa hao, Bw Collins Akenga.

Alipokuwa akijibu maswali, Bw Wamai alisema alishuku agizo hilo kwani lilikuwa na saini mbili tofauti.

Alipoulizwa na hakimu ni kwa nini alikaidi agizo hilo, alijitetea kwamba aliagizwa na kamanda wao, Bw Ipara, kutozingatia agizo hilo kwa sababu walishuku uhalali wake.

Juhudi za Bw Ipara kujaribu kumtetea afisa wake hazikufua dafu kwani hakimu huyo alishikilia kuwa afisa huyo alikuwa amekaidi amri ya mahakama na angezuiliwa hadi awafikishe washukiwa hao wawili kortini.

“Kwa heshima na unyenyekevu, tunaomba korti hii imwachilie mwenzetu kwani agizo la kwanza la mahakama liliiamuru washukiwa wazuiliwe kituoni kwa muda wa siku 14 ili uchunguzi unaoendelea ukamilike,” alirai Bw Ipara.

Licha ya hayo, mahakama ilishikilia msimamo wake wa kumzuia afisa huyo. “Nimeamuru kuwa afisa huyu azuiliwe kortini hadi pale atakapowafikisha kortini washukiwa hao. Mtu yeyote ambaye anakaidi agizo la mahakama lazima aadhibiwe,” hakimu alisema.

Maafisa wa polisi kortini walikuwa na wakati mgumu kumuamrisha mkubwa wao kuingia katika seli na badala yake wakamuacha azurure kortini wakubwa wao wakijikuna kichwa. Afisa huyo alipata afueni wenzake walipopata agizo la Mahakama Kuu kufuta agizo la hakimu.