Habari

Kizaazaa polisi wakijaribu kukamata mshukiwa mkuu wa utengezaji chang’aa Kayole

Na FRIDAH OKACHI May 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

POLISI jijini Nairobi Alhamisi usiku, walivamia na kuharibu mojawapo ya maeneo makuu ya kutengeneza na kusambaza chang’aa katika mtaa wa Soweto, eneo la Kayole, Embakasi Mashariki.

Uvamiazi huo, ulioongozwa na kikosi cha Nairobi SIERRA 2025, ulikilenga mtuhumiwa mkuu wa biashara ya pombe haramu, Bw David Nabwana maarufu kama Daudi, ambaye anadaiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika biashara hiyo haramu ya pombe mtaani Kayole.

Polisi walifanikiwa kupata lita 700 za chang’aa na kuharibu kiasi kikubwa cha busaa wakati wa operesheni hiyo.

Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Njiru, Bw John Owuoth, alithibitisha kuwa Bw Nabwana na mkewe ni watu wanaojulikana vizuri na mamlaka kwa kuhusika mara kwa mara katika utengenezaji wa pombe haramu.

Alieleza kuwa Nabwana tayari amefikishwa katika Mahakama ya Makadara mara mbili mwaka huu pekee, lakini aliachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu, jambo linalomfanya kuwa mhalifu kwa kurejelea biashara hiyo.

Kikosi cha Nairobi SIERRA 2025 kikijaribu kufungua mitungi ya kuchachua Chang’aa, Soweto, Kayole, Mei 1, 2025. Picha | Fridah Okachi.

“Leo tumeamua kufanya oparesheni kali kwa sababu pombe haramu inaharibu maisha ya watu wetu kwenye jamii na kuua. Mmiliki wa kiwanda hicho alifanikiwa kutoroka, lakini tulifanikiwa kupata lita 700 za chang’aa na tukalazimika kuharibu busaa nyingi kwa sababu ilikuwa nyingi sana kubeba,” alisema Bw Owuoth.

Wakati wa uvamizi huo pale polisi walipojaribu kumkamata Bw Nabwana, ambaye anadaiwa kuwachochea wakazi kuzuia kukamatwa kwake, jambo lililomruhusu kutoroka.

Mkewe alianzisha vurugu huku akitishia kuvua nguo kama ishara ya upinzani.

Bw Owuoth alimhimiza Bw Nabwana kujisalimisha kwenye kituo cha polisi cha Kayole, akionya kuwa msako utaendelea hadi atakapokamatwa. Pia alitoa wito kwa jamii kutojihusisha na utengenezaji wa pombe haramu, akitaja madhara yake kwa vijana na familia katika eneo hilo.

“Tunaomba wananchi waache biashara hii. Inaharibu maisha, hasa ya vijana wetu. Serikali imechukua msimamo mkali dhidi ya pombe haramu na hatutaruhusu shughuli kama hizi kuendelea,” aliongeza.

Wakazi walipongeza polisi kwa operesheni hiyo na wakaitaka kuwa ya mara kwa mara, wakisema kuwa utengenezaji wa pombe haramu huanza tena baada ya msako kukamilika.

Bi Priscilla Njoki, mkazi wa muda mrefu wa Soweto, alilalamikia madhara ya biashara hiyo kwa watoto na familia.

“Kuanzia 1998 nimekuwa nikiishi hapa. Hicho kiwanda si halali; mmiliki hana leseni yoyote ya kuendesha biashara hiyo. Hii biashara lazima ikome. Watoto wetu wanaacha shule na kuwa watoto wa mitaani kwa sababu ya pombe hii,” alisema Bi Njoki.

Mkazi mwingine alidai kuwa Nabwana hujigamba kuwa na ulinzi kutoka kwa maafisa wa juu wa polisi, na mara kwa mara hutishia kuwahamisha maafisa wanaomkabili. Alikosoa ukosefu wa uthabiti katika misako ya polisi, jambo linalotoa mwanya kwa biashara hiyo kuendelea.

“Ikiwa kweli wanataka kufunga, basi wafanye hivyo mara moja, si kufanya siku moja halafu mmiliki anarudi kuendelea na biashara. Pombe hii inauzwa mchana kutwa si usiku. Polisi wetu hupita hapa kukusanya hongo. Imeharibu ndoa nyingi na watoto hawasomi kwa sababu pesa zote zinaishia kwenye hii biashara,” alisema mkazi huyo.