KNCHR yapinga kupunguzwa kwa idadi ya makamishna wa IEBC
Na CHARLES WASONGA
TUME ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadumu (KNCHR) Jumanne imepinga pendekezo la kupunguzwa kwa idadi ya makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutoka saba hadi watano ikisema hatua hiyo itaathiri utendakazi wa tume hiyo.
Mwenyekiti wa tume hiyo Bi Kagwiria Mbogori amewaambia wabunge wanachama wa Kamati inayosimamia utekelezaji wa Katiba (CIOC) kwamba idadi ya makamishna hao inafaa kusalia saba kama ilivyo chini ya sheria ya sasa.
“Kutokana na majukumu makubwa ya IEBC kama vile uendeshaji na usimamizi wa chaguzi, uainishaji upya wa mipaka pamoja na wajibu wa kutoa ushauri kuhusu sera kuhusu aina mbalimbali za chaguzi, tume hii haifai kuwa na makamishna wanaopungua saba,” akasema Bi Mbogori kwenye wasilisho lililosomwa kwa niaba yake na mkurugenzi wa utafiti katika tume hiyo Bi Anne Okutoyi.
KNCHR imetoa mifano ya mataifa jirani ya Afrika kama vile Afrika Kusini, Malawi, Ghana, Uganda na Tanzania ambayo tume zao cha uchaguzi zina angalau makamisha saba, idadi inayolandana na majukumu ya tume hizo.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni ilikuwa ikipokea maoni na mapendekezo ya tume hiyo ya haki kuhusu mswada unaolenga kuifanyia mageuzi sheria ya IEBC kwa lengo la kupunguza idadi ya makamishna kutoka saba hadi watano.
Jopo maalumu
Mswada huo ambao uliwasilishwa bungeni mnamo Mei 5, 2019, pia unapendekeza kuundwa kwa jopo maalumu na la kudumu, la kuendesha shughuli ya uteuzi makamishna wa IEBC.
Jopo hilo pia litaendesha mchakato wa kujaza nafasi za makamishna ambao watajiuzulu kwa sababu mbalimbali kabla ya muda wao wa kuhudumu kukamilika.