Habari

Korti yaweka breki usajili wa KCSE inayoratibiwa Julai kwa wanaorudia

Na MERCY SIMIYU January 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu imesitisha kwa muda usajili wa watu wanaotaka kurudia mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) unaoratibiwa kufanywa Julai 2025.

Mahakama ya Kisii iliweka breki usajili huo kufuatia kesi iliyowasilishwa na mwanaharakati wa Nakuru Dkt Magare Gikenyi.

Jaji Teresa Odera aliagiza usajili usitishwe hadi kesi ya mwanaharakati huyo itaposikilizwa na kuamuliwa.

Dkt Gikenyi aliwasilisha kesi hiyo katika Mahakama Kuu ya Kisii akihoji kuwa hatua hiyo inakiuka haki za wanafunzi na ilichukuliwa pasipo kushirikisha umma ipasavyo.

Amewasilisha kesi akiitaka korti kufanya hima kusitisha agizo hilo kabla ya muda wa kujisajili kukamilika Februari, 21, 2025.

Dkt Gikenyi, ambaye ni mtaalamu wa upasuaji na mwanaharakati anahoji kuwa, sheria hiyo inakiuka haki za kikatiba ikiwemo haki ya kushirikisha umma.

Amedai uamuzi huo ulifanywa kiholela bila kushauriana na wadau wakuu wakiwemo wazazi na wanafunzi.

Sera mpya iliyotangazwa na Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba, Januari 8, 2025, na kurasimishwa na Knec Januari 22, 2025, inawaagiza watahiniwa wanaorudia na wale wa kibinafsi kujisajiri kwa mtihani wa Julai kati ya Januari 27 na Februari 21, 2025.

Watahiniwa wengine waliopo shuleni watashiriki mitihani yao Novemba kama kawaida.

Mlalamishi anahoji kuwa, hatua ya Knec inawakandamiza watahiniwa kwa kuwapa muda mfupi wa kujiandaa na kuunda madarasa mawili ya watahiniwa wenye ratiba tofauti za mtihani.

Anahoji kuwa, watahiniwa watanyimwa “matarajio yao ya dhati” kujiandaa na kushiriki mtihani Novemba jinsi ambavyo imekuwa ikifanyika.

Dkt Gikenyi amewashtaki Afisa Mkuu Mtendaji wa Knec, David Njeng’ere, Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, na Mwanasheria Mkuu.

Mlalamishi ameorodhesha Muungano wa Walimu Wakuu wa Sekondari (Kessha), Muungano wa Shule za Kibinafsi Nchini na Muungano wa Wazazi Nchini kama wahusika.