Habari

KRISMASI: Hali ilivyokuwa jijini Nairobi

December 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WAKAZI wa Nairobi ambao hawakusafiri kwenda mashambani walifurika katika sehemu mbalimbali za kujivinjari Jumatano kusherehekea Krismasi huku wengi wakilia kuwa hali ngumu ya kiuchumi imesambaratisha mipango yao.

Bustani ya Uhuru Park ilikuwa ni mojawapo ya maeneo ambayo watu wengi walifika kwa wingi baada ya kuhudhuria ibada ya Krismasi katika makanisa mbalimbali jijini Nairobi na maeneo ya karibu.

Wazazi na watoto wao walijivinjari huku wakishiriki michezo mbalimbali kama vile kutembezwa kwa farasi au ngamia, kuzunguka kwa mitumbwi kwenye vidimbwi, kurukaruka kwenye vibofu, kuendesha vigari  miongoni mwa michezo mingine.

Na kama kawaida walihitajika kulipa ada kabla ya kuruhusiwa na wamiliki wa vyombo hivyo vya burudani kuvitumia.

Kwa mfano, kila mtoto alitozwa Sh150 kupanda farasi na kuzungushwa kwa umbali wa mita 400 huku watu wawili wakihitaji kutoboka Sh250 kuzunguka kwa mtumbwi kwa muda wa dakika 20.

“Tunatoza ada kidogo tu ili watoto waweze kufurahia siku ya leo. Hata hivyo, baadhi ya wazazi wanalalamika kuwa ada ya Sh150 kwa mzunguko mmoja wa farasi uwanja hapa ni ghali kwa sababu uchumi ni mgumu. Lakini sisi pia tuko kazi,” akasema mwanamume aliyejitambulisha kwa jina moja, Gabriel, ambaye alikuwa akitoa huduma ya kutembeza watu kwa farasi.

Kwa upande mwingine wahudumu wa vibofu walikuwa wakitoza ada ya Sh100 kwa muda wa dakika 20 kwa kila mtoto. Michezo hiyo na ile ya kubingiria ndani ya kibofu (balloon) majini ilionekana kuwavutia watoto wengi zaidi.

Na wasanii wa kuchora nyuso za watoto hawakuachwa nyuma kwani wao pia walivuna pakubwa. Bi Maria Wanjiku alisema alikuwa analipisha kati ya Sh50 na Sh200 kulinga na michoro ambayo mzazi angependelea.

“Kando na hayo ninawauzia vibofu (balloon), miwani na toys (mwanasesere) kwa bei nafuu ili nao weweze kufarahia kuzaliwa kwa Yesu Kristo,” akasema mfanyabiashara huyo ambaye anaishi mtaa wa Kayole.

Biashara za peremende, barafu, soda, maji ya chupa, mayai na vitafunio vinginevyo nayo ilinoga katika bustani ya Uhuru Park.

Hata hivyo, watu wengi walilalamikia hatua ya baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa hizo. Kwa mfano, soda ndogo ya mililita 300 iliunzwa kwa Sh50 badala ya bei ya kawaida ya Sh30.

Waliojenga vibanda vya kupigia picha, vilivyowekwa mapambo na maandishi yanayohusiana na Krismasi nao walivuna pakubwa kwani alipata wateja kemkem. Walipiga Sh100 kwa nakala mbili za picha ambazo hutolewa hapo hapo.

Nao wezi walitumia mandhari hiyo ya msongamamo wa watu kuiba simu na vibeti katika bustani hiyo.

Hata hivyo, wale ambao hawakuwa na bahati walijipata pabaya kwani walipewa kichapo cha mbwa kabla ya kuwasilishwa kwa maafisa wa polisi ambao walishika doria katika eneo hilo.

Wakati huo huo, barabara za katikati mwa jiji ambazo kawaida huwa na misongamano ya watu na magari zilisalia mahame kwani maduka mengi hayakuwa yamefunguliwa.

Uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali ulibaini kuwa katika barabara za Moi Avenue, Kimathi Street, Koinange Street na Kenyatta Avenue biashara nyingi zilikuwa zimefungwa isipokuwa maduka ya Supermarket ambayo ndiyo yalikuwa yamefunguliwa.