Habari

KRISMASI: Mamia wakwama

December 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

MAMIA ya wasafiri waliokuwa wakielekea maeneo ya mashambani kwa sherehe za Krismasi walikwama majiji ya Nairobi na Mombasa kwa kukosa magari ya kuwasafirisha, na pia nauli ya juu iliyotozwa na wahudumu wa magari yaliyopatikana.

Jijini Mombasa, biashara ilinogea kampuni za mabasi kufuatia idadi kubwa ya wasafiri wanaoelekea bara kwa ajili ya sherehe hizo.

Taifa Leo ilipozuru vituo vya mabasi jijini humo ilishuhudia misongamano mikubwa ya watu huku wengi wakipigania kupata nafasi kwenye mabasi hayo.

Jijini Nairobi, baadhi ya wahudumu waliongeza nauli kwa hadi Sh1,600, hivyo kuwalazimu baadhi ya abiria kuahirisha safari zao.

Abiria waliokuwa wakisafiri kuelekea maeneo ya Kisumu, Bungoma na Busia walikuwa wakilipishwa Sh2,600 kutoka nauli ya kawaida ya Sh1,000 huku waliokuwa wakielekea Kericho na Eldoret wakitozwa kati ya Sh2,000 na Sh2,200 kutoka nauli ya kawaida ya Sh800.

Wale wanaoishi maeneo ya karibu na Nairobi pia hawakusazwa, kwani walijipata katika hali hiyo hiyo. Waliokuwa wakienda Machakos walikuwa wakitozwa Sh400 kutoka wastani wa Sh200, huku waliokuwa wakielekea maeneo ya Kitui na Mwingi wakitozwa kati ya Sh800 na Sh1000 kutoka wastani wa Sh400.

Magari ya kuelekea Kisii yalikuwa yakiwatoza abiria kati ya Sh1,500 na Sh2,200 kutoka wastani wa Sh1,000.

Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa wale ambao walikata tiketi zao mapema, kwani wengi wao walikuwa wakilipa nauli za kawaida au kuongezewa kati ya Sh200 na Sh300.

Katika steji ya Afya Centre ambapo magari ya kuelekea Kisii huchukua abiria, waliotaka kusafiri walikuwa wakipigania magari.

Kulingana na Edna Moraa, ambaye alikuwa akielekea Kisii, alilazimika kulipa Sh2000 kutoka Sh1,000 baada ya kuchelewa kukata tiketi.

“Nimelazimika kulipa kiasi hicho kwani tuliambiwa kwamba magari yaliyopo ni machache na yote yamekatiwa tiketi,” akasema Moraa, ambaye alikuwa amefika kituoni humo saa kumi alfajiri.

Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa Emily Njoroge, aliyesema kwamba alilipa nauli ya Sh1,000 baada ya kukata tiketi mapema. “Nilijua mapema msongamano huu ungetokea, ndipo nikaamua kukata tiketi mapema,” akasema.

Misongamano ya watu na magari pia ilishuhudiwa katika steji za Railways, Nyamakima, Tea Room na Machakos Country Bus.

Uchunguzi wetu pia ulibaini kwamba baadhi ya magari yanayohudumu jijini Nairobi pia yalikuwa yakiwasafirisha abiria nje ya jiji hadi katika sehemu kama Kisumu, Kisii na Magharibi mwa nchi.

Dereva mmoja ambaye hakutaja kutajwa alisema kuwa walikuwa wamepata kibali cha kuhudumu nje ya jiji msimu huu. Hata hivyo, baadhi ya wasimamizi wa kampuni za usafiri waliwalaumu abiria kwa kukata tiketi zao wakiwa wamechelewa.

“Msongamano tunaoshuhudia ni kutokana na abiria wanaokuja dakika za mwisho mwisho kukata tiketi. Haingekuwa hivi ikiwa wangezilipia mapema,” akasema Eric Ong’era, anayesimamia Mabasi ya Guardian, yanayosafiri kuelekea jijini Kisumu.