Habari

Krismasi ya msoto

December 24th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

CHANGAMOTO tele zilizowakumba Wakenya mwaka huu zimefanya wengi wakose mpango wa kufurahia sherehe za Krismasi kutokana na ukosefu wa fedha.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la TIFA Research, changamoto kubwa ambazo Wakenya wamepitia zinajumuisha ukosefu wa ajira, gharama kubwa ya maisha na umaskini, mbali na ufisadi unaolaumiwa kwa kuzorotesha uchumi.

Hayo yamefanya wengi wao kupanga kutumia kiasi kidogo cha fedha kwa shamrashamra za Krismasi ikilinganishwa na jinsi walivyofanya mwaka uliopita.

“Nchini Kenya, Krismasi ni mojawapo ya sikukuu kubwa zaidi ambapo wananchi hutumia fedha nyingi na muda mwingi kusherehekea. Huwa wanapanga kusafiri kujumuika na jamaa zao,” ripoti hiyo inaeleza.

Ripoti ya utafiti huo iliyotolewa Jumatatu inaonyesha kwamba asilimia 42 ya Wakenya wanapanga kutumia fedha ndogo msimu huu, tofauti na walivyofanya 2018.

Kwa upande mwingine, kuna asilimia 33 pekee ambao walisema wataongeza kiwango cha fedha watakazotumia, lakini kuna wengine asilimia 11 ambao hawana mpango wa matumizi yoyote maalumu wakati wa Krismasi.

Utafiti huo uliofanywa kati ya Desemba 17 na 22, kupitia mahojiano ya simu umebainisha kwamba asilimia 60 ya Wakenya wanapitia hali ngumu zaidi ya kifedha ikilinganishwa na walivyokuwa mwaka uliopita.

Ni asilimia 21 pekee ambao walipohojiwa walisema hali yao ya kifedha imekuwa bora mwaka huu.

Kimaeneo, ni wakazi wa eneo la Kaskazini Mashariki pekee ambao idadi yao kubwa (asilimia 70) walisema hali yao kifedha imeboreka mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 26 ya waliolalama kuhusu hali mbaya.

Eneo la Mashariki ya Kenya liliongoza kwa idadi kubwa ya Wakenya ambao wanakumbwa na hali ngumu kifedha (asilimia 78), likifuatwa na eneo la Kati (asilimia 65), Magharibi (asilimia 64) na Nyanza (asilimia 62).

Katika eneo la Pwani, ni asilimia 45 pekee ya waliohojiwa ambao walisema hali imekuwa mbaya zaidi mwaka huu, huku Nairobi kukiwa na asilimia 54, na Rift Valley asilimia 56.

Kuhusiana na matumizi ya fedha msimu huu wa Krismasi, ripoti hiyo ilibainisha kuwa matumizi makubwa zaidi yatakuwa katika ununuzi wa vyakula.

Hii itafuatwa na kiwango cha fedha kitakachotumwa kwa wazazi na jamaa wengine, mavazi, usafiri na makao ya muda kama vile mikahawa na vyumba vya wageni.

Kwa wastani, Wakenya wanaopanga kutumia fedha wakati wa sikukuu watatumia Sh5,103 (kwa wastani) kununua vyakula, na Sh5,045 kutuma kwa wazazi na jamaa.

Wakenya pia wamepanga kutumia Sh4,132 kwa ununuzi wa mavazi, na Sh3,112 kwa usafiri na makazi ya muda.

Maeneo ya Kaskazini Mashariki, Kati, Nyanza na Rift Valley yaliongoza kwa idadi ya watakaotumia fedha zaidi kwa vyakula.

Kiwango cha juu zaidi cha fedha kitatumiwa kuwatumia wazazi na jamaa katika maeneo ya Pwani, Mashariki, Nairobi, Rift Valley na Magharibi.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa, kiasi kidogo zaidi cha fedha kitatumiwa kwa usafiri na kugharamia makao ya muda na wakazi wa maeneo ya Kati, Pwani, Mashariki, Nairobi, Nyanza, Rift Valley na Magharibi.

Utafiti huo ulifanywa kwa kuhoji Wakenya wenye umri wa kati ya miaka 18 na 45 kutoka maeneo yote manane ya Kenya ambayo yalikuwa mikoa zamani. Asilimia 51 ya waliohojiwa walikuwa wanawake, na asilimia 49 wanaume.