Kulikoni baadhi ya viongozi wa Jubilee walia eti wamepokonywa walinzi?
Hilo ndilo swali lililokuwa kwenye vinywa vya wengi Ijumaa baada Gavana wa Kiambu Ferdinard Waititu Babayao na mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa kudai kupokonywa walinzi bila kupewa sababu na serikali.
Taifa Leo, hata hivyo, ilibaini kuwa idadi ya wabunge walioathiriwa na hatua hiyo ya serikali huenda ni ya juu.
Uamuzi huo unaonekana kulenga viongozi wa vuguvugu la Tanga Tanga, linalounga mkono Naibu wa Rais William Ruto kuwania urais 2022 Rais Kenyatta atakapostaafu.
Bw Babayao aliambia Taifa Leo kwamba, yeye pamoja na Bw Ichungwah walipokonywa walinzi.
“Kweli, walinzi wangu pamoja na wa Bw Ichung’wah wameondolewa bila kupewa sababu,” akasema Bw Babayao kupitia arafa.
Gavana Babayao, hata hivyo, hakujibu alipoulizwa ikiwa amewasilisha malalamishi kwa Idara ya Polisi kuhusiana na hatua hiyo ya serikali au la.
Bw Ichung’wah ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti, alikuwa nje ya nchi alipopokonywa walinzi.
Bw Ichung’wah kwa sasa yuko nchini Amerika kwa shughuli rasmi za bunge.
Lakini mbunge huyo wa Kikuyu alithibitisha kuwa amepokonywa walinzi huku akidai kwamba hatua hiyo inalenga kumshinikiza kuacha kuunga mkono Dkt Ruto.
“Ni kweli, wamenipokonya walinzi wangu. Hatua hiyo ni ya kisiasa na inalenga kunishinikiza nisifanye kazi na Naibu wa Rais William Ruto,” Bw Ichung’wah akaambia Taifa Leo kupitia arafa.
Akaongezea: “Siko nchini lakini Mungu anajua wanachopanga kunifanyia.”
Owino akanusha
Msemaji wa Polisi Charles Owino, hata hivyo, alikanusha madai kwamba viongozi hao wamepokonywa walinzi huku akisema hayo ni mabadiliko ya kawaida katika idara ya polisi.
Bw Owino alisema polisi wa kawaida wanaolinda watu mashuhuri wameondolewa na mahali pao patachukuliwa na Polisi wa Utawala (AP).
“Hakuna mtu atapokonywa walinzi. Kinachoendelea ni mabadiliko ya kawaida. Polisi wa AP ndio wamepewa jukumu la kulinda watu mashuhuri,” akasema Bw Owino.
Alisema kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Rais Kenyatta yanataka polisi wa AP kutekeleza mahukumu muhimu kama vile kulinda miundomsingi, usalama wa mipaka na kulinda watu mashuhuri.
Mbunge wa Kipkelion Magharibi Hillary Koskei aliambia Taifa Leo kuwa hana habari kuwa serikali imempokonya walinzi wake.
Alithibitisha kuwa yeye angali na walinzi wake.
“Mbunge anapochaguliwa ana haki ya kupewa walinzi bila kujali mrengo wa kisiasa anaoegemea,” akasema Bw Koskei.
Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Laikipia, Catherine Waruguru hakuthibitisha ikiwa amepokonywa wakulinzi au la na badala yake alitutaka kutafuta kauli kutoka kwa wizara ya Usalama.
“Nani anasema kwamba tumepokonywa walinzi? Andikieni Wizara ya Usalama iwape majibu,” akasema Bi Waruguru kupitia arafa.