Habari

Kuppet yataka walimu wapewe mafunzo ya kijeshi

January 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA FAITH NYAMAI

CHAMA cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (Kuppet), kimetoa wito kwa serikali itoe mafunzo ya kijeshi na kuwapa bunduki walimu wanaohudumu maeneo ya Kaskazini Mashariki na Pwani mashambulizi ya kigaidi mara kwa mara.

Katibu Mkuu wa Kuppet, Akelo Misori pia ameshutumu Wizara ya Usalama kwa kuzembea katika kuwahakikishia walimu wa maeneo hayo usalama wao.

Bw Misori, ambaye alikuwa akirejelea mauaji ya walimu watatu waliovamiwa eneo la Kamuthe, Kaunti ya Garissa mapema wiki hii, alisema watumishi wa serikali ndio hulengwa zaidi na Al Shabaab kwa sababu huwana silaha za kujikinga.

“Kila shule au chuo Kaskazini Mashariki lazima kilindwe na maafisa wa polisi. Wakati pia umetimia kwa serikali kutoa mafunzo ya kijeshi kwa walimu na iwape bunduki ndipo wajilinde dhidi ya Al Shabaab,” akasema Bw Misori.

Afisa huyo wa Kuppet aliongeza kwamba uvamizi dhidi ya walimu mara nyingi hutekelezwa na Al Shabaab nyakati za usiku wakati polisi hawako karibu na shule.

“Walimu walipovamiwa, walionusurika walisimulia jinsi polisi walikataa kufika kuwasaidia wakidai kwamba lazima wasubiri hadi asubuhi ndipo wakabiliane na wavamizi hao,” akasema Bw Misori.

Chama hicho pia kimetoa wito kwa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) iangazie upya sera za utoaji ajira ili kuhakikisha walimu wanaoajiriwa katika Kaunti za Garissa, Mandera, Wajir, Tana River na Lamu ni wazaliwa wa maeneo hayo.

Vilevile Bw Misori alitangaza kuwa amemwandikia barua Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i akimwomba ahakikishe kuwa polisi wawili wanatumwa kulinda kila shule inayopatikana maeneo yenye utovu wa usalama.

“Watu waliosomea taaluma ya elimu ambao wameajiriwa kwenye idara za jeshi na polisi wanafaa watumwe kufundisha katika shule za maeneo hayo. Walimu hao wanafaa kusalia wanajeshi na wapewe bunduki huku pia wakifundisha,” akasema Bw Misori.

Mwenyekiti wa Kuppet, ambaye pia ni mbunge wa Emuhaya, Omboko Milemba naye alitaka TSC ipunguze miaka ambayo walimu wanaofundisha kwenye maeneo yanayoshambulia na magaidi huchukua kabla ya kupewa uhamisho.

Walimu hao hufundisha kwa miaka mitano kabla ya kuhamishwa na sasa Bw Milemba anataka muda huo upunguzwe hadi miwili.