MWAKA huu ulianza na imani kuwa Kenya ilikuwa imepiga hatua kutoka kwa majanga yaliyotokana na kuenezwa kwa itikadi kali za kidini ambayo ilitokea Shakahola mnamo 2024.

Mauti ya watu 450 Shakahola yalihusishwa na imani yenye itikadi kali iliyokuwa ikiendelezwa na Paul Nthenge Mackenzie ambaye yuko korokoroni Shimo La Tewa na washirika wake.

Serikali chini ya Rais William ilitangaza msitu wa Shakahola kama eneo la uhalifu na sasa ipo chini ya ulinzi mkali wa zaidi ya maafisa 30 wa polisi kwa saa 24 huku Mackenzie aliyejirejelea kama mhubiri akiendelea kusota korokoroni.

Hatua hiyo ililenga kuhakikisha kuwa hakuna mazishi yanayoendelezwa kisiri kwenye msitu huo.

Wizara ya Usalama wa Ndani iliwahakikishia Wakenya kuwa haitavumilia na kuruhusu maafa ya Wakenya kutokana na itikadi kali ya kidini.

Mackenzie na washirika wake wakiwa korokoroni na pia usalama kuimarishwa Shakahola, Wakenya walifikiria kuwa sasa kila kitu kiko sawa.

Mnamo Julai mwaka huu, mambo yalibadilika baada ya makaburi yenye kina kifupi kupatikana Kwa Bi Nzaro ambayo ni kilomita 30 kutoka makaburi yaliyopatikana ndani ya msitu wa Shakahola.

Baada ya wiki mbili ya kuchimba, makachero kutoka Idara ya Upelelezi Nchini (DCI), wahudumu wa mochari na Wanapatholojia, walifukua miili 32 na pia mingine 102 ambayo ilikuwa imeoza na kuchanganyika na mchanga.

Mauti yaliyopatikana Kwa Bi Nzaro yalishangaza nchini jinsi tu yalivyokuwa yale ya Shakahola.

Uchunguzi ulibaini kuwa baadhi ya manusura na waliohepa oparesheni iliyokuwa ikiendelezwa Shakahola ndio walikusanyika ndani ya Ranchi ya Chakama Kwa Bi Nzaro.

Huko waliendelea kufunga hadi kifo na kuwazika wale ambao walikuwa wamekufa. Watu 11 walikamatwa na idadi ya washukiwa wakuu walipunguzwa hadi wanne, wakiwa ni Sharleen Temba Anindo, aliyejiita nabii pamoja na washirika wake Kahindi Kazungu Garama, Thomas Mukonwe na James Kahindi Kazungu.

Uchunguzi ulibaini wanne hao walikuwa sehemu ya waumini wenye itikadi kali Shakahola na waliendelea na shughuli zao baada ya kuhepa msituni.

“Namjua Bi Anindo, alikuwa jirani yangu Shakahola lakini sijui kwa sasa yuko wapi,” akasema Shahidi Robert Kithi mahakamani.

Alisema hayo mapema mwezi huu wakati ambapo kesi ya Mackenzie ilikuwa ikiendelea kuhusiana na mauti ya watoto 191.

Mauti ya Shakahola na Kwa Bi Nzaro yanaonyesha jinsi itikadi ilivyozonga familia nyingi na kusababisha mauti ya wapendwa.

Serikali ina kibarua kigumu kukabili hadaa hii ili kuwaokoa Wakenya ambao wanaendelea kuumia kutokana na kufumbwa macho na imani potovu.