Kwa nini tunapinga BBI
Na BENSON MATHEKA
MSWADA wa kubadilisha katiba kupitia mchakato wa maridhiano, maarufu kama BBI, una njama fiche ya kurejesha nchi katika utawala wa kidikteta, viongozi na wanaharakati wanaoupinga wanaonya.
Kulingana na kiongozi wa Narc Kenya, Martha Karua, ambaye ametangaza kuwa ataupinga, nia ya kubadilisha katiba sio kuunganisha Wakenya na kuboresha maisha yao inavyodaiwa, bali ni kuficha udhaifu wa serikali iliyo mamlakani.
Juhudi za kubadilisha katiba zilianza na handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, na Bi Karua anasema kwamba, walitumia njia za mkato zinazoweza kurejesha utawala wa kidikteta ilivyokuwa wakati wa utawala wa chama cha Kanu.
“Uhuru Kenyatta na Bw Odinga wanafaa kujua kwamba, hatutarudi katika udikteta. Hatufai kuruhusu damu, jasho na machozi ya Wakenya waliopigana na kuondoa udikteta wa Kanu kupotea bure,” alisema.
Alisema ingawa mchakato huo umevumishwa kama wa kunufaisha Wakenya, unapatia rais mamlaka makubwa zaidi.
Kulingana na mswada huo, Rais atakuwa na nguvu za kuteua na kufuta waziri mkuu na manaibu wake. Mawaziri watakuwa wabunge hatua ambayo wanaopinga mswada huo wanasema itapokonya bunge uhuru iliyopewa na katiba ya 2010.
Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekanusha kwamba mswada huo utarejesha enzi za rais mwenye mamlaka makubwa.
“Ni kuhalalisha udikteta kupitia mchakato ambao sio wa kikatiba,” asema Bi Karua.
Anasema kwamba mabadiliko yaliyoleta udikteta nchini ikiwemo kuanzishwa kwa sehemu ya 2A iliyoanzishwa 1991 yalinuiwa kupatia rais nguvu nyingi. “Lengo la mchakato wa BBI sio tofauti na mabadiliko hayo,” alisema.
Kulingana na Bi Karua, lengo la BBI ni kufunika maovu ya serikali kama vile kupuuza katiba ya 2010 na kukosa kuitekeleza na ufisadi.
“Tunataka kuwaambia Wakenya kwamba mapendekezo ya BBI yananuiwa kuficha na kuhalalisha makosa na udhaifu wa viongozi wa sasa na sio kutatua shida hata moja inayokabili mwanachi wa kawaida,” alisema.
Gavana wa Makueni, Kivutha Kibwana anasema mbali na kupatia Rais nguvu zaidi, BBI itawafanya Wakenya kuwa masikini zaidi kwa sababu ya nyadhifa zaidi za uongozi na viti vipya vya wabunge.
“Ninapinga BBI kwa sababu itaumiza mwananchi wa kawaida. Wananchi ambao wanalemewa na umasikini watabebeshwa mzigo wa kulipa mishahara ya viongozi zaidi,” asema.
Mswada wa BBI unapendekeza kubuniwa kwa maeneobunge mapya 70 ambayo yataongeza viti vya ubunge kutoka 290 hadi 360. Ukipitishwa, seneti itakuwa na maseneta 94 waliochaguliwa badala ya 47. Pamoja na wawakilishi wa kuteuliwa, idadi ya wabunge itakuwa zaidi ya 500.
Profesa Kibwana pia anasema kwamba, mchakato huo ulitekwa na wanasiasa wanaolenga kulinda maslahi yao 2022 bila kujali mateso watakayolimbikizia Wakenya.
“BBI inahusu 2022. Hakuna mabadiliko ambayo Wakenya watapata na wanaopenda nchi yao wanafaa kukataa BBI,” alisema.
Ingawa magavana wenzake wameunga mapendekezo hayo wakisema yataimarisha ugatuzi kwa kuwa kaunti zitatengewa pesa zaidi, Profesa Kibwana anasema inahitaji baraza la mawaziri kupitisha kaunti zipatiwe asilimia 35 ya mapato ya serikali bila kubadilisha katiba.
Kulingana na wakili wa masuala ya kikatiba PLO Lumumba, mapendekezo mengi katika BBI hayahitaji mabadiliko ya kikatiba bali yanahitaji sheria za kuyatekeleza kubuniwa na bunge.
“Kwa maoni yangu, mapendekezo haya ni mpango wa wanasiasa wa kuongeza nyadhifa za uongozi. Yanalenga kuficha nia halisi ya wanasiasa,” asema.
Mtaalamu huyu anasema kubuniwa kwa nyadhifa hakutatua shida ya ukosefu wa ujumuishaji katika serikali.
Anasema kinachohitajika kuimarisha ugatuzi sio kutengea serikali za kaunti mbali ni kugatua majukumu.
Akizungumza katika kipindi kimoja cha runinga ya mtandao, Bw Lumumba alisema kuna uwezekano wa BBI kukataliwa na Wakenya.
“BBI sio wazo baya lakini mbinu inayotumiwa kuiendesha ndiyo mbaya na kuna uwezekano wa kukataliwa kwenye kura ya maamuzi,” alisema.
Bi Karua anaonya kuwa ikiwa BBI itapita, wanasiasa watakuwa wamepokonya Wakenya sauti na mamlaka yao.
Aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga anaonya kuwa, huenda BBI ikafungua milango ya kuvuruga katiba ya 2010 iliyopatia Wakenya matumaini.
“Ushauri wangu kwa Wakenya, na hasa vijana ni kuwa, huenda wasiwe na nchi katika muda wa miaka 10 ijayo mtindo huu ukiendelea,” alisema.