Lalama kuhusu mazingira mabovu ya usahihishaji KCSE
Na OUMA WANZALA
SHUGHULI ya kusahihisha mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE 2019) imekumbwa na hali mkanganyiko baada ya usahihishaji wa somo la biashara kutatizika kwa siku ya pili sasa wasahihishaji wakilalama.
Wasahihishaji 700 wa KCSE shuleni Machakos High tayari walikuwa wameagizwa na wasimamizi wa vitu kuondoka jana Jumatatu – ikiwa hawaridhiki – baada ya kulalama siku mbili kuhusu mazingira mabovu ya kazi, haya yamethibitishwa na katibu mkuu wa chama cha walimu wa shule za upili na asasi za elimu ya juu (Kuppet) Bw Akelo Misori.
Shughuli hiyo ilianza Jumamosi shuleni Machakos lakini walimu hao hawafurahishwi na malipo ya Sh46 kila nakala wanayosahihisha kulinganishwa na Sh68 walizotaka wawe wakilipwa kwa kila nakala.
Wasahihishaji hao zaidi ya 700 wamelalama kuwa wamelazimika kulala sakafuni pakabu kukiwa na baridi kali.
Mapema leo Jumanne, maafisa wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (Knec) wamekutana na wasahihishaji hao na kukubali kuboresha malipo kuwa Sh52 kila nakala, ingawa hawajaridhika.
Knec imesema inatupa mpango wa kuwataka waondoke ikikumbatia majadiliano badala yake.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Knec, Bi Mercy Karogo amesema Jumanne kwamba suala hilo limetatuliwa.
“Tumeketi tukajadiliana kuhusu suala hili lilitishia kulemaza shughuli ya usahihishaji,” amesema Dkt Karogo.
Shughuli hiyo ilianza Jumamosi ambapo walimu 26,597 wanashiriki katika vituo 20 jijini Nairobi na viunga vyake na inatarajiwa kutamatika katikati mwa Desemba 2019.