Lazima katiba ibadilishwe, Raila asisitiza
ELISHA OTIENO na RUTH MBULA
KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, ametaka wale wanaopinga marekebisho ya katiba wakae kando na kuachia wananchi nafasi ya kujiamulia kuhusu wanavyotaka kuongozwa.
Akizungumza Alhamisi akiwa Kaunti ya Migori, Bw Odinga alisema wakati umefika kwa katiba kurekebishwa na hakuna kitakachozuia hilo.
“Huwezi kuzuia utekelezaji wa jambo ambalo wakati wake umefika,” akasema mjini Awendo, alipoongoza kampeni za Bw Ochillo Ayacko anayewania useneta kupitia ODM.
Kulingana naye, katiba za nchi nyingi ulimwenguni hubadilishwa baada ya angalau miaka minane hivyo basi haistahili watu waseme bado ni mapema kwa katiba iliyopitishwa 2010 kufanyiwa marekebisho.
“Ni lazima tufanye utathmini wa kama ugatuzi umetufaa, na kutatua changamoto ibuka kupitia kwa marekebisho ya sheria. Tujiulize kama serikali kuu ina uwakilishi mkubwa kupita kiasi, na pia masuala ya kimazingira,” akasema.
Baadhi ya viongozi akiwemo Naibu Rais William Ruto, wamekuwa wakipinga marekebisho ya katiba.
Wamekuwa wakidai kuwa Bw Odinga na wenzake wanashinikiza marekebisho ya katiba ili waingie serikalini kupitia nyadhifa mpya zitakazobuniwa kama vile Waziri Mkuu na manaibu wake.
“Wale wanaopinga suala hili ni kama vilio vya chura ambavyo havitazuia ng’ombe kunywa maji,” akasema.
Alipozungumza mjini Rongo ambapo aliandamana na Gavana wa Siaya Cornel Rasanga, Naibu Gavana wa Kisumu Mathew Owili, Kiongozi wa Wachache Bungeni John Mbadi na wabunge mbalimbali, waziri huyo mkuu wa zamani alisema jopo alilounda na Rais Uhuru Kenyatta limepiga hatua katika majukumu yake.
Alisema wanachama wa jopo hilo wataanza kuzunguka nchini hivi karibuni kukusanya maoni ya wananchi kuhusu jinsi ya kutatua changamoto zinazokumba taifa.
Kuhusu uteuzi wa moja kwa moja wa Bw Ayacko ambao ulisababisha mgawanyiko miongoni mwa wanachama wa ODM katika kaunti hiyo, alisema chama kiliamua hivyo kwa sababu Bw Ayacko ndiye alipatikana kuwa bora zaidi miongoni mwa waliotaka tikiti ya ODM.
“Tulifanya kura ya maoni akaibuka mshindi na pia uzalendo wake kwa chama umedumu kwa muda mrefu,” akaambia umati.
Uteuzi wa Bw Ayacko ulimfanya Gavana wa Migori Okoth Obado kuasi chama hicho na kumuunga mkono Bw Eddy Oketch, 27, wa chama cha Federal Party of Kenya.
Bw Odinga amekita kambi katika kaunti hiyo kwa siku mbili kabla uchaguzi mdogo wa useneta ufanywe Jumatatu.
Bw Oketch ameonyesha upinzani mkali dhidi ya Bw Ayacko kufikia sasa na amekuwa akitumia helikopta kwenye kampeni zake mbali na rasilimali nyingine za bei ghali.
Mwanasiasa huyo kijana alipuuzilia mbali madai ya baadhi ya viongozi wa ODM waliodai anafadhiliwa na Bw Ruto, akasema rasilimali anazotumia sasa ni zile zile alizoruhusu viongozi hao kutumia wakati wa kampeni za urais mwaka uliopita kwa hivyo waache unafiki.