Maafa ya mvua yasambaa
Na WAANDISHI WETU
JANGA la mafuriko limeendelea kusababisha maafa na vilio katika maeneo ya Nyanza, Magharibi, Nairobi, Mashariki na Pwani.
Katika Kaunti ya Kisumu, familia 600 zimelazimika kuhama makwao baada ya Mto Nyando kuvunja kingo zake kufuatia mvua inayoendelea kunyesha katika nyanda za juu za Vilima vya Nandi.
Wakazi wa vijiji vya Kakola-Ombako na Kano-Kabonyo jana waliamkia mafuriko ya kutisha ambayo yalisomba mimea na maji kujaa katika nyumba zao.
Nyumba 90 zilisombwa katika vijiji vitatu katika eneo la Kariwindi Kusini na zingine 50 katika maeneo ya Kanyipola na Kasambura-Kamahawa.
Baadhi ya wenyeji walionekana wakiwanusuru mifugo yao na mali nyingine kwa kutumia boti huku wengine wakijitosa majini kuokoa chochote ambacho wangeweza.
Katika eneo la Nyatike, Kaunti ya Migori, familia kadhaa zimesalia bila makao na sasa zimelazimika kukita kambi kwenye makanisa na afisi ya chifu.
Katika Kaunti Kisii, watu wanne walikufa maji katika maeneo mbalimbali ya sehemu hiyo.
Idara ya kukabiliana na majanga imewaonya wakazi wa wadi tano katika kaunti hiyo wawe macho huku Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ikitoa tahadhari kwamba mvua kubwa itaendelea kushuhudiwa maeneo mengi.
Wadi hizo ni Moticho na Bomariba katika eneobunge la Mugirango Kusini, Boikanga kwenye eneobunge la Bonchari na wadi za Nyatieko na Monyerero katika eneobunge la Kitutu Chache Kusini.
“Tunawaomba wakazi katika wadi ambazo tumezitambua wahamie maeneo ya juu ili kuzuia majanga wakati huu wa mvua nyingi,” akasema Alex Nyamweya ambaye ni afisa wa kusimamia kitengo cha utoaji wa huduma za dharura.
Katika eneo la Pwani, zaidi ya watu 300 katika kaunti ndogo ya Voi, Kaunti ya Taita Taveta waliachwa bila makao usiku wa kuamkia jana baada ya Mto Voi kufurika na kuvunja kingo zake kufuatia mvua kwenye vilima vya Wundanyi na Mwatate.
Walioathirika ni wenyeji wa vijiji vya Gimba, Msambweni na Tanzania. Wenyeji hao waligutuka mwendo wa saa tisa alfajiri baada ya nyumba zao kufurika licha ya kuwa eneo lao halikuwa likinyesha.
Watu hao walikumbwa na mkasa huo ghafla na wengi hawakuweza kuokoa mali yao iliyosombwa na maji.
Shirika la Msalaba Mwekundu liliendelea na shughuli ya kutafutia waathirika makao. Tayari kuna watu kadhaa ambao wamepata makao katika shule ya chekechea ya Tanzania.
Mwanaisha Hamisi alisema kuwa serikali inajitahidi angalau waathiriwa wapate chakula na mahali pa kulala.
Katibu wa kaunti hiyo, Bw Liverson Mghendi alisema mkasa huo ulisababishwa na uchimbaji wa changarawe.
Katika jiji la Nairobi na viunga vyake, barabara nyingi zilijaa maji na zilizoathirika zaidi ni katika maeneo ya Westlands, South C, Thika Road, Parklands na Kilimani.
Katika Kaunti ya Makueni, maafisa wa uokoaji walimuokoa mwanaume wa miaka 35 aliyekuwa ameripotiwa kusombwa na maji alipokuwa akijaribu kuvuka Mto Kaiti.
Na IAN BYRON, BENSON AYIENDA, ELIZABETH OJINA, DIANA MUTHEU, LUCY MKANYIKA, AMINA WAKO Na PIUS MAUNDU