Maandamano kona zote Kenya
Na WAANDISHI WETU
WANANCHI wengi waliochoshwa na matatizo yanayowakumba kimaisha Jumanne waliandamana katika pembe tofauti za nchi wakitaka serikali iache kupuuza kilio cha walala hoi.
Kutoka maeneo ya Pwani hadi Magharibi ya nchi, raia walijitokeza wakiwa na aina tofauti za malalamishi, mengi yakihusu matukio yanayowasababishia ugumu wa hali ya maisha wakihisi serikali imewasahau.
Katika Kaunti ya Mombasa, mamia ya wakazi waliandamana hadi katika Bunge la Kaunti kuwasilisha malalamishi yao kuhusu maagizo ya usafirishaji mizigo kwa reli mpya ya SGR.
Maandamano hayo yamekuwa yakifanywa kila Jumatatu lakini wiki hii yalifanywa Jumanne kwa kuwa Jumatatu ilikuwa likizo.
“Tarehe mbili Novemba tutaanzisha vuguvugu la Okoa Mombasa. Sote tutatoka kimasomaso tuokoe Mombasa,” akasema Bw Francis Auma ambaye ni mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu.
Waandamanaji hao walilalamika kwamba tangu walipoanza maandamano yao, viongozi wa kaunti wamejitenga nao na badala yake kuungana na serikali kuu kutoa ahadi ambazo hazitekelezwi huku raia wakiumia.
Katika Kaunti za Nairobi, Uasin Gishu na Kakamega, vijana waliohusika katika shughuli ya kuhesabu watu kitaifa mnamo Agosti waliandamana wakisema hawajalipwa hadi sasa.
“Kazi hiyo ilikuwa ngumu sana. Tulifanya kazi hadi usiku wa manane. Sisi ni vijana lakini tunahangaishwa. Tunastahili kupewa haki yetu na tulipwe kwani tulifanya kazi ilivyohitajika,” akasema Bw Ibrahim Musa, ambaye alihudumu katika Kaunti Ndogo ya Turbo, Uasin Gishu.
Taharuki sawa na hii ilishuhudiwa katika eneo la Mumias, Kaunti ya Kakamega wakati wakulima wa miwa walipoamua kuandamana wakilalamikia kucheleweshwa kwa ripoti ya jopokazi lililochunguza changamoto zinazokumba sekta hiyo.
Wakulima hao walisema walitumai ripoti hiyo ingesaidia kutoa mwelekeo ambao ungesaidia kusuluhisha vikwazo vya sekta ya sukari vilivyofanya viwanda vingi kufilisika na hivyo kuwaacha wakulima katika umaskini.
Jopokazi hilo lililosimamiwa na Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri na Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya lilikuwa limebuniwa Novemba mwaka uliopita kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta, na lilistahili kutoa ripoti yake baada ya miezi sita iliyokamilika Mei.
“Tunapoendelea kuzungumza kuhusu kuboresha sekta ya sukari, hali inazidi kuwa mbaya. Tunahitaji suluhisho kuhusu hatua zinazofaa kuchukuliwa kufufua sekta hii haraka iwezekanavyo,” akasema Bw Ali Wangalwa, mmoja wa wakulima.
Katika eneo la Mlima Elgon, Kaunti ya Bungoma, jamii za Ogiek na Ndorobo ambao wanaishi maeneo yanayopakana na Msitu wa Chepkitale waliandamana kulalamikia mipango ya kuwafurusha eneo hilo.
Kutembea
Walitembea kutoka soko la Chebyuk hadi makao makuu ya Kaunti Ndogo ya Kopsiro wakilalamika kwamba kuna wanasiasa wanaotaka wafurushwe ili kujinufaisha kisiasa ilhali eneo wanakoishi si sehemu ya msitu.
“Tunataka ifahamike wazi kwamba Chepkitale haijawahi kuwa sehemu ya msitu wa Mlima Elgon,” akasema msemaji wao, Bw Amos Kisa Sanutia.
Maandamano mengine yalifanyika katika Kaunti ya Samburu ambako wanawake wakiongozwa na viongozi wa kike wa kisiasa walilalamikia ukosefu wa usalama katika eneo la Baragoi, Samburu Kaskazini.
Walisema wanawake ndio huathirika zaidi kutokana na mauaji eneo hilo.
Imeripotiwa na Valentine Obara, Edith Chepng’eno, Ken Wamasenu, Dennis Lubanga na Shaban Makokha