HabariSiasa

Maandamano Murang'a baada ya Nyoro kukamatwa

September 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NDUNGU GACHANE na CHARLES WASONGA

SAA chache baada ya mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro kukamatwa Jumatatu jioni katika Kanisa la Kianglikana (ACK) la St James Cathedral Kaunti ya Murang’a, maandamano yalizuka mjini Murang’a kupinga kukamatwa kwake.

Wakazi walionekana wakichoma magurudumu katikati ya barabara kuonyesha ghadhabu zao na kusimama na mbunge wao aliyekamatwa na maafisa 50 wa GSU kuhusiana na fujo zilizovuruga mkutano wa mchango wa fedha katika Kanisa Katoliki la Gaitu Jumapili.

Waandamanaji hao waliwakejeli polisi kwa kile walitaja kama kuteswa na kutishwa kwa mbunge wao ambaye amekuwa akieneza siasa za Tangatanga.

“Tutazidi kumuunga mkono mbunge wetu kwa kuwa analengwa na serikali kwa sababu zisizo na mashiko,” wakasema wakazi hao.

Afisa wa Upelelezi wa Jinai katika kaunti ya Murang’a Julius Rutere alisema Nyoro atashtakiwa kwa kosa la kuzuia polisi kumkamata, kushambulia polisi na kuvuruga ibada ya kanisa.

Mbunge huyo amezuiliwa katika kituo cha polisi cha Murang’a kusubiri kuwasilishwa mahakamani Jumanne. Wakili wake Irungu Kang’ata ndiye mtu wa kipekee ambaye ameruhusiwa kumwona.

Katika fujo za Jumapili mbunge huyo na Mbunge Maalum Maina Kamanda walijibizana vikali wakati wa harambee hiyo huku Bw Nyoro akisisitiza ni yeye alipasawa kupewa nafasi ya kuongoza shughuli hiyo “kwa sababu mimi ndiye mbunge aliyechaguliwa hapa Kiharu.”

Bw Nyoro ni mwanachama wa kundi la Tangatanga ilhali Bw Kamanda ni mwanachama wa kundi la Kieleweke, makundi hasimu ndani ya chama tawala cha Jubilee ambayo yanatofautiana kuhusu siasa za urithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Mapema Jumatatu, jumla ya maafisa 50 wa polisi walipiga kambi katika Kanisa la ACK St James Cathedral ambako Bw Nyoto na wabunge; Peter Kamari (Mathioya) na Muturi Kigano (Kangema) walikuwa wakishiriki katika kipindi kwenye runinga moja inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kikuyu.

Kufuatia fujo iliyoshuhudiwa katika Kanisa Katoliki la Gaitu Jumapili , Dayosisi ya Murang’a ya Kanisa hilo sasa limepiga marufuku harambee zinazoongozwa na wanasiasa katika makanisa yake.

Amri hiyo ilitolewa na Askofu James Maria Wainaina kufuatia ushauri wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Nchini Kadinali John Njue.